Gwiji wa Simba SC Zamoyoni Mogella amesema timu yake hiyo ya zamani imepoteza hali ya kujiamini, na kukubali kupoteza alama tatu muhimu mbele ya Young Africans ambayo inaendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mogella aliyetamba na wekundu hao wa Msimbazi mwanzoni mwa miaka ya 1980 mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1990 amesema Simba SC wangeweza kupata ushindi kwenye mchezo dhidi ya Young Africans lakini wamepoteza hali ya kujiamini.
Amesema wamekosa nafasi nyingi za kufunga kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambazo kama wangezitumia vizuri wangeweza kuwaweka Young Africans kwenye wakati mgumu.
“Wamepoteza hali ya kujiamini kwa kuwa Young Africans ni bora kwa sasa na kutokana na hilo walijikuta wakikosa nafasi nzuri za kufunga hasa kipindi cha kwanza na ambazo kama wangefanikiwa kuzitumia, wangewaweka Young Africans kwenye wakati mgumu wa kushinda mechi hiyo,” amesema Mogella
Amesema Simba haina nafasi tena ya kushinda ubingwa msimu huu kwa sababu mechi zimebaki chache na Young Africans wako kileleni kwa tofauti ya pointi nyingi na kuwashauri wajipange kwa ajili ya msimu ujao.
“Hawana cha kufanya kwa sasa kushinda ubingwa. Wajipange kwa msimu ujao, kwa jinsi ilivyo na ubora wa Young Africans sio rahisi kupoteza mechi nyakati kama hizi na zaidi wako mbele kwa tofauti ya pointi nyingi” amesema Mogella aliyewahi pia kuitumikia Young Africans.
Young Africans walibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC juzi Jumamosi (Aprili 20) na kuendelea kuongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 58 kwenye mechi 22 walizocheza.