Binadamu ni neno lenye asili ya Kiarabu linalomaanisha “Mwana wa Adamu”, ana mambo sana huyu kiumbe lakini ukiachilia mbali muunganiko wa lugha ili waweze kuelewana, pia kuna tamaduni mbalimbali ambazo zinawaweka pamoja na kukuza maelewano yao, ikijumuisha mila na desturi katika kila kitu kinachowazunguka ikiwemo tabia.
Ulimwengu huu ni tajiri wa kila kitu na ndio maana pia kuna maelfu ya tamaduni tofauti tangu mwanzo wa uumbaji, lakini kinachoshangaza ni utamaduni wakiojiwekea ambao wengine hufanya ni kanuni kuu zinazotakiwa kufuatwa na kila mtu aweze kuzitii kulingana na eneo husika.
Kwa mujibu wa mtandao wa ncbi.nlm, Duniani kuna tamaduni zaidi ya 3800 za kipekee, zikiwemo zile za kuzoeleka na zingine si za kushangaza lakini zipo zile ambazo ukizisikia tu, basi ni lazima zitakushangaza lakini kwa jamii husika yenyewe hujivunia na kuziheshimu, kuzithamini na kuziendeleza vizazi na vizazi.
Hapa nakuletea baadhi ya tamaduni ambazo zinaweza kukufanya uungane nami kushangaa kwamba je? inawezekanaje jambo hili, lakini kwa wahusika wao wanachukulia ni jambo la kawaida na ni sehemu ya kuendeleza kila wanachokiamini na yeyote anayeenenda kinyume basi huchukuliwa tofauti na wakati mwingine kuwajibishwa.
1. Kupumzika makaburi – Denmark.
Katika nchi nyingi, Makaburi huchukuliwa kama ni sehemu ya kuogofya, lakini Nchini Denmark wao ni tofauti kwani wamejiwekea utaratibu wa kwenda kupumzika maeneo hayo. Makaburi mengi ya Nchi nyingi yamepambwa vizuri na hutembelewa na wengi wakati wa majira ya joto.
Ukitaka kuamini hili waweza ulizia au kufuatilia Makaburi ya ‘Assistens Cemetery’ yaliyopo katika mji mkuu wa nchi hiyo Copenhagen, yenyewe ni kithibitisho tosha kwani ukifika hapo utakuta watu wametandika virago vyao wamepumzika huku wakijisomea vitabu, kupiga soga huku wakijiburudisha kwa vinywaji na vitafunwa.
2. Siku ya kupeana ujauzito – Urusi.
Septemba 12, 2006 Rais wa Urusi, Vladimir Putin alihutubia taifa hilo na kutangaza janga la idadi ndogo ya watu kuwa ni tatizo la dharura na akatangaza jitihada za kuongeza kiwango cha idadi ya watu na kuongeza uzazi nchini Urusi.
Putin pia alisema Serikali ingetoa motisha ya pesa taslimu kwa familia ambazo zina zaidi ya mtoto mmoja, ili zihamasike kuongeza watoto, ndipo siku hiyo ya Septemba 12 kila mwaka ikawa ni siku muhimu ambayo ilipewa heshima kama ‘siku ya kupeana ujauzito kwa raia wa Urusi.
Badaye Serikali ikaanzisha siku ya mapumziko kwa umma, ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kuwapa wanandoa muda wa faragha kwa matumaini kwamba watashika mimba na Wazazi ambao watoto wao huzaliwa miezi tisa baadaye wakapewa fursa ya kushinda zawadi na Watoto wanaozaliwa Septemba 12 hupata zawadi kutoka kwa Mamlaka.
3. Salamu ya mabusu – Ufaransa.
Kupiga busu ni jambo kama la kawaida katika jamii nyingi hasa za Magharibi, lakini kupiga busu kila mtu na kwa idadi zaidi ya mara moja na kila wakati ni utamaduni uliozoeleka, yaani ukikutana na mtu uwe unamjua ama humjui we ukikutana naye unampa mabusu ‘dabo dabo’ huo ni utamaduni wa salamu wa kawaida kabisa nchini Ufaransa.
Katika taifa hilo ili uonekanae umemthamini mtu na kumsabahi, ni muhimu kumpiga busu na unavyombusu mara nyingi zaidi basi hiyo huonesha thamani yake na namna unavyomuheshimu zaidi, ingawa kuna tofauti ya busu kati la Wanaume na Wanawake.
Namna unavyomsubu Mwanamke ama Mwanaume kunatofautina na pia idadi ya busu zinazohitajika hukamilisha mabadiliko ya salamu hiyo na unatakiwa kusalimiana na kila mtu kwenye sherehe au mkusanyiko baada ya wageni kuwasili, iwe unawajua au la, hivyo ukifika Ufaransa jiandae kupigwa mabusu mengi na jitayarishe kupiga mabusu mengi bila kuanziasha ugomvi. Lakini nitoe tahadhari kwa Wabongo ni Busu tu jamani.
4. Kulala kifudifudi kama heshima – Nigeria.
Hii kibongobongo ni ngumu sana, lakini kwa Wanigeria ni kawaida, wao kulala kifudifudi kama kwa jamii ya wayoruba ni ishara ya heshima mbele ya wakubwa zako, hili ni kabila ambalo limechukua sehemu kubwa nchini Nigeria.
Mila ya kulala kama salamu inachukuliwa kwa ni ya uzito mkubwa hasa wakati wa kuwasalimia wazee ama watu wazima, tofauti na ilivyozoeleka hapa kwetu kwa kupiga magoti lakini kwa ndugu zetu hawa Wayoruba, kijana kulala chini kabisa na kuweka uso chini ni ishara ya utii kwa wakubwa.
Hata hivyo kuna utaratibu wa salamu hii, ipo hivi kwa Mabinti wao hupiga magoti wakati wa kusalimiana na kwa Wanaume wao hulala kifudifudi, ikiwa ni ishara ya heshima kwa wazee katika jamii na utamaduni huo ndiyo huwatofautisha Wayoruba na makabila mengine nchini Nigeria.
5. Kuonyesha kitu kwa ishara ya midomo – Nicaragua.
Hii kwa hapa kwetu huwa tunatumia sana kidole au mkono na imezoeleka sana kwa kabila mbalimbali au tuseme maeneo mengi ni hivyo Duniani lakini si katika Taifa la Nicaragua, kwani wao huonesha ishara kwa kutumia midomo badala ya kidole kama watu wengi walivyozoea duniani.
Midomo inatumika kwa ishara ya kukubaliana kitu, kuonyesha kitu ama njia ya kukupa ujumbe, hivyo basi unatakiwa kuwa makini sana pale unapokuwa kwenye mazungumzo na Mnicaragua kwa kumtazama na kumfuatilia kwa ukaribu kwenye midomo yake kuweza kumuelewa usisubiri mikono yake utafeli.
Waweza kustaajabia lakini nikuhakikishie tu kwamba wenyewe wanaelewana vizuri na ni kitu kinachowatambulisha kwa ukaribu katika kijamii yao hivyo kama utabahatika kwente katika Nchi hiyo uwe umejipanga na ukirudi pia kumbuka sisi tunatumia mkono au Vidole hivyo usichanganye mambo.