Imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Manchester United Erik ten Hag amepoteza imani kwa Wajumbe wa Bodi wa klabu hiyo, na huenda akafungashiwa virago mwishoni mwa msimu huu 2023/24.

Gazeti la The Sun la England limeeleza kuwa, Kocha huyo kutoka nchini Uholanzi alikuwa akipata utetezi kutoka kwa baadhi ya Wajumbe wa Bodi, ambao waliamini akipewa muda anaweza kufanya jambo la tofauti, lakini kwa sasa hali imekuwa ndivyo sivyo.

Sare ya 3-3 dhidi ya Coventry City, kabla ya Man Utd kushinda kwa mikwaju ya Penati kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la FA mwishoni mwa juma lililopita, imekuwa chanzo cha imani ya Ten Hag kuzidi kufifia klabuni hapo.

Mbali na Bodi kupoteza imani na Kocha Ten Hag, The Sun wameripoti kuwa shinikizo lingine la kocha huyo kuondolewa Man Utd linatoka kwa baadhi ya mashabiki ambao wamekuwa wakichukizwa na mwenedo wa kikosi chao.

United walikuwa mbele kwa mabao 3-0 zikiwa zimesalia dakika 20 kumalizika, lakini iliteleza na kujikuta ikikubali kuipa nafasi Coventry City iliyosawazisha mabao hayo na nusura ipoteze mchezo kwa mabao 4-3 katika muda wa nyongeza.

Wenyeviti wenza Avram na Joel Glazer walikuwa kwenye mchezo huo na mwekezaji mpya Sir Jim Ratcliffe, ambaye sasa anadhibiti shughuli za michezo za klabu hiyo.

TFS wapeleka tumaini jipya la Vijana kiuchumi Rufiji
Barabara ya Jangwani yafungwa, huduma mwendo kasi zasimama