Kiungo kutoka nchini England na klabu ya Real Madrid Jude Bellingham ameweka wazi matarajio yake msimu huu 2023/24, huku akipanga kutwaa mataji matatu.
Bellingham alisajiliwa na Real Madrid mwaka jana ‘2023’ akitokea nchini Ujerumani alipokuwa akiitumikia Klabu ya Borussia Dortmund.
Kiungo huyo usiku wa kuamki leo Jumanne (Aprili 23) alitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo za Dunia za Laureus za 2024, sambamba na nyota wa Tenisi wa Hispania Carlos Alcaraz.
Bellingham amesema amedhamiria kutwaa mataji matatu msimu huu 2023/24, mawili akiwa na Klabu yake ya Real Madrid, na moja akiwa na timu ya Taifa lake la England.
Hadi sasa Real Madrid ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa Ubingwa wa Ligi ya Hispania ikiongoza msimamo wa Ligi ya nchi hiyo ‘La Liga’ kwa kufikisha alama 81, ikifuatiwa na FC Barcelona yenye alama 70, huku kila timu ikicheza michezo 32 hadi sasa.
Katika hatua nyingine Real Madrid imetinga hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ‘UEFA Champions League’ kwa kuifunga Manchester City 4-3 kwa mikwaju ya Penati katika mchezo wa mkondo wa pili wa Robo Fainali.
Kwa upande wa England, Bellingham amejiwekea matumaini ya kuwa sehemu ya wachezaji watakaoliwezesha taifa hilo kutwaa Ubingwa wa Fainali za Mataifa ya Barani Ulaya ‘EURO 2024’.
“Bila shaka ni jambo ninalotaka kulifanya,” alisema Kiungo huyo akiwa katika zulia jekundu baada ya kutwaa tuzo yake katika usiku wa Tuzo za Dunia za Laureus huko mjini Madrid.
“Bado tuna mechi chache zaidi za kumaliza La Liga na kisha tuna mechi mbili ngumu sana dhidi ya Bayern Munich katika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.
“Kwa Euro 2024, England tumejipanga kutwaa Ubingwa wa michuano hiyo, kwani msimu uliopita wa Fainali hizi tulifika hatua ya Fainali na tukapoteza dhidi ya Italia kwa Penati.”
Bellingham tayari amefunga mabao 21 katika mechi 36 alizoichezea Real katika michuano yote msimu huu, baada ya kukamilisha uhamisho wa Euro milioni 103 kutoka Borussia Dortmund msimu uliopita wa majira ya Kiangazi.
Washindi wengine katika Tuzo za Laureus ni pamoja na Mchezaji namba moja kwa ubora dunia kwenye mchezo wa Tenis Novak Djokovic, Mwanasoka wa kikosi cha Wanawake cha Hispania na Klabu ya Baracelona Aitana Bonmati na Mchezaji Sarakasi kutoka nchini Marekani Simone Biles.