Waziri wa Nch, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemevu, Deogratus Ndejembi amewataka wajiri wote ambao hawajajisajili na OSHA wafanye usajili haraka iwezekanavyo, ili kujikinga na athari zinazojitokeza mahali pa kazi.
Akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Jijini Dodoma kuhusu siku ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi itakayofanyika Aprili 28, 2024 amesema kuna umuhimu mkubwa katika kujisajili na kwamba wataanza kufanya ukaguzi, ili kubaini waajiri ambao hawajajisajili.
Amesema, “hatutomvumilia yoyote yule ambae hatojisajili na OSHA kwasababu wanahatarisha maisha ya wafanya kazi katika eneo la kazi na hivi karibuni tuanza kufanya ukaguzi, ili kubaini waajiri ambao hawajajisajili, na pia waajiriwa mna haki ya kutoa taarifa kama taasisi unayofanyia kazi haijajisajili, tutakuwa wakali.”
Hata hivyo Ndejembi amebainisha kuwa, hivi karibuni OSHA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataanza kampeni ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa OSHA na pia athari za kutojisajili na madhara yanayoweza kujitokeza kiusalama mahali pa kazi ili Watanzania wajifunze.
“Takwimu za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani mwaka 2022 zinaonesha kwamba zaidi ya watu 2,900,000 hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo, zaidi ya wafanyakazi 4,200,000 huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi wanachopatiwa matibabu,” amesema.
Ndejembi ameongeza kuwa, “kwa upande wetu hapa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249. Katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217.”