Ukiukwaji wa haki za binaadamu unazidi kushamiri duniani kote, huku hali inazidi kuwa mbaya kwa zaidi ya miongo kadhaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuenea kwa serikali za kimabavu ambazo zinaharibu utaratibu wa kimataifa kwa kukiuka sheria na kutojali haki za kimsingi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, imeeleza kuwa pia migogoro ya Gaza na Ukraine inachangia na kwamba vitendo viovu dhidi ya raia na unyanyasaji unaokosa utetezi vimekuwa ni sababu tosha.
Katibu Mkuu wa shirika hilo, Agnès Callamard amesema pia kuongezeka kwa migogoro, matumizi silaha na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wa Sudan, Ethiopia na Myanmar aumekuwa ukizidi kuondosha amani ya raia wengi na kwamba jitihada za kimataifa zinahitajika kukomesha hali hiyo.
Aidha, ripoti hiyo pia inakosoa matumizi ya Marekani ya kura yake ya turufu ambayo imepelekea kulemaza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, juu ya azimio la kusitisha mapigano Gaza.