Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), Almasi Kasongo amesema ligi hiyo itamalizika Mei kama ilivyopangwa pamoja na mabadiliko madogo ya ratiba.

Akizungumza Dar es Salaam, Kasongo alisema kurejea kwa mashindano ya Kombe la Muungano kumesababisha mabadiliko madogo kwenye ratiba ya baadhi ya mechi kwenye Ligi Kuu.

“Unaweza kuona kwenye ratiba yetu ya mwaka 2023/24 hatukuweza kuingiza ratiba ya mashindano haya, tumelazimika kufanya hivyo sasa.

“Msimu ujao ratiba yetu itaingiza na mashindano ya Kombe la Muungano ili kuondoa usumbufu wowote unaoweza kujitokeza kutokana na kurejea kwa mashindano haya,” amesema Kasongo.

Ameongeza: “Haya mabadiliko kwa namna yoyote ile hayawezi kuathiri tarehe ya mwisho tuliyopanga ligi kumalizika, hivyo ligi itafikia kikomo Mei 29 kama ilivyopangwa”.

Ligi ya Muungano imerejea baada ya zaidi ya miaka 20 tangu ilipochezwa kwa mara ya mwisho mwaka 2003 na inaanza leo Jumatano (Aprili 24) kwa mchezo kati ya Simba SC na KVZ ya Zanzibar Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kesho Alhamis (Aprili 25) Azam FC itacheza na mabingwa wa Zanzibar, KMKM kwenye uwanja huo huo na fainali yake itachezwa Aprili 27.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Zanzibar ‘ZFF’, Hussein Ahmada amesema mashindano hayo yatasaidia kukuza kiwango cha soka kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

“Kupitia mashindano haya vipaji vipya vitavumbuliwa ambavyo vitatumia kwa manufaa ya timu ya taifa kwenye mashindano mbalimbali.

Mwaka huu, tumefanya uzinduzi tu na mwakani watu watarajie mabadiliko makubwa kwenye mashindano haya ya kihistoria,” amesema

Amewaomba mashabiki wa mchezo wa soka visiwani humo kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo kuongeza ushindani zaidi.

Serikali za mabavu chanzo ukiukwaji haki za Binadamu
Gwiji Young Africans achekelea kiwango