Uongozi wa Singida Fountain Gate FC, umesema bado unatambua Mlinda Lango Beno Kakolanya ni mali yao halali, lakini hatima yake itajulikana ndani ya saa 72 kuanzia jana Jumanne (Aprili 23).
Kupitia Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Massanza, amesema suala la hatua gani itamchukulia Mlinda Lango huyo ni baada ya Kamati ya Nidhamu itakapokutana na kujadili suala lake.
Kauli hiyo imekuja baada ya Mlinda Lango huyo kugomea wito wa kamati hiyo ambayo ilitakiwa kukutana naye Aprili 19, mwaka huu, kwa ajili ya mahojiano na kumpa nafasi ya kujieleza.
Mlinda Lango huyo hakutokea katika kikao hicho na baadaye kuandika barua kwa kamati hiyo kuwa viongozi walifanya makosa ya kutoa tuhuma kuwa anaihujumu timu hiyo kwa kitendo cha kuondoka kambini kwa ruhusu ya Meneja wa timu.
Imeelezwa Mlinda Lango huyo ameondolewa katika Group (kundi) la mtandao wa kijamii la wachezaji ambalo anaweza kupata taarifa mbalimbali za klabu hiyo.
Massanza amesema hatma ya Mlinda Lango huyo adhabu au atasamehewa ni hadi kamati hiyo itakapokutana leo na ndani ya saa 72 watatoa maamuzi yao, lakini hadi sasa wanatambua Kakolanya bado ni mchezaji wao halali.
“Suala la kuondolewa katika group la timu na amekuja Mwanza kuchukuwa vitu vyake sifahamu, mchezaji wao halali ninachafahamu ni kwamba kipa huyo hayupo kambini kabla ya kucheza mechi yetu dhidi ya Young Africans, suala la adhabu gani atachukuliwa baada ya kugomea wito ni maamuzi ya kamati,” amesema Massanza.
Hata hivyo, chanzo chetu ndani ya klabu hiyo kilisema Mlinda Lango huyo ameondolewa moja kwa moja ndani ya kikosi hicho baada kutuhumiwa kuwa anahujumu timu hiyo, hivi karibuni walipokuwa wakicheza na Young Africans mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alipotafutwa Kakolanya ameeleza sababu ya kutokwenda kwenye kamati hiyo baada ya kupokea Barua ya wito wa Kamati ya Nidhamu Aprili 19, mwaka huu, aliipeleka kwa mwanasheria wake (hakumtaja jina), ambapo alimshauri wanapaswa kuwajibu kwanza.
“Mwanasheria wangu akaipitia vizuri Sana, baada ya hapo aliniambia lazima tuwajibu kwani kuna makosa Singida Fountain Gate FC wameyafanga kwa kutoa hukumu kupitia ukurasa wao na kurasa zingine kubwa za mitandao ya kijami.
“Kwa hiyo nikaandika barua ya kutokuhudhuria kwenye kikao cha kamati ya nidhamu kwa kuwa tayari wameshanihukumu hivyo hata nikienda kwenye kikao kitakuwa si halali na ni kinyume cha sheria.
Wao walitakiwa waniite kwanza wanisikilize kabla ya kutoa hukumu kwa hiyo kwenye kikao hicho nisingepata haki yangu ya msingi.” Amesema Mlinda Lango huyo.