Kocha Mkuu wa KenGold, Jumanne Chale ameelezea kufurahishwa kwake na timu hiyo kupanda Ligi Kuu soka Tanzania Bara.

Timu hiyo yenye maskani yake Wilaya ya Chunya, Mbeya itaungana na timu nyingine mkoani humo ya Tanzania Prisons kwenye, Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Tayari Bodi ya Ligi Kuu Soka Tanzania (TPLB) imeitambua KenGold kuwa timu ya kwanza kutoka ligi Championship kupanda Ligi Kuu huku kukisalia mchezo mmoja ligi hiyo kukamilika.

“Nina furaha kwa sababu tumefanikiwa kufikia malengo yetu ya kuipandisha timu Ligi Kuu msimu ujao. Ni heshima kubwa kwa mkoa mzima wa Mbeya kwa sababu ni kama wamepata mtoto wa pili. Lakini kama unavyofahamu kupata mtoto sio tatizo, kazi ngumu ni kumtunza mtoto mwenyewe.

“Kwa hiyo nawaomba watu wote wa mkoa huu kujitokeza kuiunga mkono timu hii iweze kukabiliana na presha ya kushiriki Ligi Kuu msimu ujao,” amesema Chale.

KenGold wamepanda Ligi Kuu baada ya kufikisha pointi 67 wakishinda mechi 20, kutoka sare mara saba na kufungwa mechi mbili huku wakiwa wamesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Polisi Tanzania Uwanja wa Sokoine, Mbeya Jumamosi (Aprili 27).

Hata hivyo kazi kubwa ya kupanda msimu ujao imebaki kwa Pamba FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 64 na Mbeya Kwanza ina pointi 62.

Kwenye mchezo wa mwisho Pamba FC watakuwa wageni wa Mbuni Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Mbeya Kwanza wataikaribisha Transit Camp Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Manji: Sina mpango wa kurudi Young Africans
Singida FG yamng’ang’ania Kakolanya