Shujaa wa Everton Dominic Calvert-Lewin amesema ushindi wao dhidi ya Liverpool ni wa kipekee sana, na unapaswa kubaki katika kumbukumbu ya msimu huu 2023/24.
Mshambuliaji huyo alifunga bao la pili na la ushindi kwa Everton kwenye mchezo dhidi ya Liverpool uliopigwa usiku wa kuamkia leo Alhamis (Aprili 25), katika Uwanja wa Goodison Park, huku bao la kwanza likifungwa na Jarrad Paul Branthwaite.
Baada ya kuiwezesha Everton kuchukuwa alama tatu muhimu dhidi ya Liverpool Calvert-Lewin amesema: “Ushindi wetu dhidi yao ni maalum zaidi, ni Dabi ya ndani na nimekuwa hapa kwa muda wa kutosha kujua maana yake kwa mashabiki na maana yake kwangu.
“Ni matokeo mazuri kutokana na mazingira tuliyopo kwenye ligi. Tulihitaji alama tatu kubwa na kila kitu kilikuja pamoja usiku wa jana.”
Kuhusu morari kutoka kwa mashabiki wa Everton ambao walichangia kupatikana kwa ushindi huo, Calvert-Lewin ameongeza: “Nguvu yao ilikuwa kama umeme. Wakati wote walitimiza wajibu wao, na imetusaidia kufikia lengo la kupata ushindi.
“Ni uzoefu mzuri na kumbukumbu nzuri kwa kila mtu. Ni jambo ambalo tutaangalia namna ya kuliendeleza ili tumalize vizuri msimu huu.”