Johansen Buberwa – Kagera.
Takribani Wanawake 347 wamebainika kuwa na maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi, kati ya wanawake 4689 waliyofanyiwa uchunguzi wa maradhi hayo Mkoani Kagera.
Mganga Mkuu wa Mkoa Kagera, Dkt. Samwel Laizer ameeleza hayo katika kilele cha chanjo Afrika kimkoa, kilichofanyika Manispaa ya Bukoba kwa kuambatana na uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV).
Dkt. Laizer amesema Mkoa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayoathiriwa na magonjwa yanayodhibitiwa kwa chanjo ikiwemo saratani ya mlango wa kizazi kwasababu takwimu za mwaka 2023/2024 zinaonesha kiwango kikubwa cha ongezeko la wagonjwa wa saratani ya HPV.
“Kwa mwaka 2023 zinaonyesha wanawake waliyofanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa 17668 na kubaini kuwa wanawake 469 wana mambukizi ya ugonjwa huo na mwaka huu kwa kipindi cha January 2024 wanawake 4689 wamefanyiwa uchunguzi na kubaini 347 kuwa na maambukizi ya HPV,” alisema.
Naye Abdoni Kawha ambaye alimwakilishi Afisa Elimu Mkoa Kagera kwenye uzinduzi wa wa chanjo ya HPV, amesema jumla ya Wanafunzi 17600 kutoka shule 362 watashiriki chanjo hiyo na wamejipanga vizuri kuhakikisha walengwa wote kutoka shule hizo wanafikiwa kama ilivyo mpango wa Serikali.
Hata hivyo, Mratibu wa chanjo Mkoa Kagera, Salimu Rajab Kimbao amesema wamepokea dozi 299,040 ambazo tayari wamezifikisha katika vituo vyote vya afya Mkoani humo kwa ajili ya kuwakinga walengwa wote na kwa kila Halmashauri uzinduzi unaendelea na huduma ya kutoa chanjo ukiwa unanalenga kufikia asilimia 90.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Bukoba Erasto Sima, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Kagera Hajath Fatma Mwasa amewataka wataalamu wote watakaohusika kwenye zoezi hilo kuhakikisha wanafika kwenye vituo na maeneo waliyopangiwa kufanya kazi pamoja na kusimamia na kutumika vifaa ipasavyo.