Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Gamondi, amesema licha ya kuwapo kwa ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, wachezaji wake wamekuwa wakipambana uwanjani kusaka alama kwa dakika zote kwa ajili ya kufikia malengo yao, jambo ambalo linampa matumaini makubwa ya kutetea ubingwa wao, lakini hawajawa na uhakika kwa asilimia 100.
Young Africans juzi Jumamosi (Aprili 27) waliendelea kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea Ubingwa wao baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kufikisha alama 64 kileleni, bao hilo pekee likifungwa na Joseph Guede.
Gamondi amesema mechi ilikuwa ngumu sana licha ya kutokea mambo mengi ndani ya Uwanja ikiwamo kutopewa Penati pamoja na kutengeneza nafasi nyingi kwa kushindwa kuzitumia, lakini wachezaji walipambana na kufanikiwa kupata bao hilo la ushindi.
“Tulicheza mpira mzuri, nimefurahi wachezaji walitulia na kufanikiwa kukusanya alama tatu kwa bao pekee la Guede, mchezaji mzuri na mshambuliaji wa mwisho amefanya kazi nzuri.
“Kuhusu Bacca (lbrahim), si majeruhi bali nilifanya mabadiliko ya safu ya ulinzi kwa kumpumzisha kwa sababu ya kucheza mechi nyingi na mfululizo kulingana na jinsi ya ratiba ya ligi ilivyo kwa sasa,” amesema Gamondi.
Ameeleza kuwa wako kwenye nafasi nzuri ya kutwaa taji la ubingwa, lakini bado hawajakuwa na asilimia 100 kwa hilo kwa sababu bado wana michezo mkononi na ligi haijaisha, hivyo wanatakiwa kuwa makini kusaka ushindi bila kuangalia waliopo chini yao wanafanya nini.
Naye Kocha Mkuu wa Coastal Union Kocha Mkuu, David Ouma, amesema wachezaji wake walicheza vizuri licha ya Young Africans kuwa na wachezaji wazoefu ambao waisaidia kufanikisha ushindi huo.
Amesema Young Africans walipata alama tatu wakiwa pungufu baada ya mchezaji wake (Lawi) kupewa kadi nyekundu, hali ambayo wapinzani wao hao walitumia nafasi hiyo kupata bao moja.
“Sio mchezo nzuri kwangu kwa sababu tulipoteza, ninaimani tungekuwa kamili wasingetufunga, kipindi cha kwanza tukiwa 11 kwa 11 hawakupata nafasi ya kufunga hadi dakika 69 tulienda 0-0 baada ya kadi nyukundu ndio wakatufunga,” amesema Ouma.
Ameongeza kuwa mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa kwa timu zote mbili na anawapongeza wachezaji wake kufanya kile alichokielekeza kwenye uwanja wa mazoezi na kuhamisha uwanjani.