Klabu ya Pamba Jiji FC imeshauriwa kufanya usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa umakini mkubwa kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu na ubora wa kucheza ligi hiyo.

Hayo yamesemwa na winga wa zamani wa timu hiyo, Khaleed Bitebo wakati wa mahojiano katika Uwanja wa Nyamagana jijini hapa.

Bitebo ameipongeza Pamba Jiji FC kwa kurejea Ligi Kuu Tanzania ikiwa ni takribani miaka 25 tokea iliposhuka.

“Pamba Jiji FC ina mashabiki wengi ni wakati sasa wa viongozi wa timu kuwa na umoja na mshikamano. Kamati ya usajili inatakiwa kufanya usajili wa makini sana,” amesema

Bitebo amesema timu nyingi zilizopanda Ligi Kuu msimu uliopita zimepata changamoto kutokana na aina ya usajili waliofanya.

Ameitahadharisha Pamba Jiji FC kuhusu kuchukua wachezaji wa kigeni wakati Tanzania kuna wachezaji wengi wazuri na wenye ubora mkubwa.

Ameishauri Kamati ya Usajili ya Pamba Jiji kushirikisha wachezaji wa zamani wa klabu hiyo kupata ushauri wa nini chakufanya.

Amesema Pamba Jiji FC iepuke kuchukua makocha wanaokuja na wachezaji wao wasio na uwezo, bali wachague wachezaji wazuri kuimarisha timu hiyo.

Naye winga wa zamani wa Pamba FC, Venance Kazungu amesema Pamba Jiji inatakiwa ifanye usajili wenye mvuto ili timu iwe bora kama zamani.

Katika msimamo wa Ligi ya Championship iliyomalizika juzi Jumapili (Aprili 28), Pamba Jiji FC imemaliza katika nafasi ya pili ikiwa na alama 67 baada ya michezo 30 iliyocheza.

Hersi amaliza uvumi wa Pacome
Rais Samia: Mradi bonde la Mto Msimbazi kupunguza athari za mafuriko