Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Hersi Saidi amemaliza uvumi uliozagaa kuwa mchezaji wao Pacome Zouzoua hana vibali na huenda klabu hiyo ikafungiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Aidha, uvumi huo pia ulidai Young Africans huenda ikapokonywa pointi zote ilizopata ilipomchezesha mchezaji huyo katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza Dar es salaam, Saidi amesema uvumi huo umemuibua Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliyetaka kujua ukweli sababu za kutocheza Pacome, huku wengine wakivumisha kuwa sababu hana vibali.
Amesema mchezaji huyo hana tatizo lolote ana vibali vyote vinavyomruhusu kucheza soka nchini, zikiwemo leseni za CAF na FIFA, kibali cha kazi na kile cha kuishi nchini.
Amesema alikuwa kando kwa ajili ya maumivu tu na wala hakukuwa na jambo jingine.
Aidha, Saidi amesema kikubwa wanataka Young Africans kuwa miongoni mwa timu bora kabisa Afrika huku akisisitiza kuwa wanataka pia mwakani kucheza katika mashindano ya klabu ya dunia.
Amesema mwakani kutakuwa na timu nne zitakazokwenda katika mashindano hayo ya klabu ya dunia, hivyo Young Africans itakuwa miongoni mwa timu nne za Afrika zitakazoshiriki mashindano hayo msimu unaofuata.
Amesema Young Africans imepiga hatua kubwa kwani msimu uliopita ilicheza Fainali ya Kombe la Shirikisho na msimu huu imefikia Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya miaka 25, na hiyo imewaongezea pointi katika viwango vya ubora.
Akizungumzia kuhusu kuwa tayari kumuuza nyota wao Aziz Ki, Saidi amesema katika hali ya kawaida kama unataka kufanya vizuri lazima uendelee kuwa na wachezaji wako, ikishindikana unamuuza kwa bei nzuri na mwisho unanunua mchezaji sahihi atakayeziba pengo hilo.
Akihojiwa na Yanga TV, Pacome mwenyewe amesema anaendelea vizuri na anaweza kucheza mchezo ujao wa Young Africans wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma, Mei 5.