Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imetupilia mbali ombi la dharura la Shirikisho la Soka la Algeria na Klabu ya USM Alger la kubatilisha matokeo ya mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya USM Alger dhidi ya RS Berkane.
CAF iliipa ushindi wa 3-0 RS Berkane kufuatia mchezo wa Mkondo wa kwanza uliotakiwa kufanyika nchini Algeria, kutokana na jezi za klabu hiyo kuzuiwa Uwanja wa Ndege kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kisiasa.
Mchezo wa Mkondo wa Pili uliotakiwa kuchezwa mwishoni mwa juma lililopita nchini Morocco nao haukuchezwa kufuatia timu ya USM Alger kugoma kuingia katika eneo la kuchezea licha ya kufika Uwanjani.
Kwa mantiki hiyo RS Berkane imetinga Fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu 2023/24 na itachezeza dhidi ya Zamalek ya Misri iliyofanikia kuitoa Dream FC ya Ghana kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.
Mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali Kombe la Shirikisho umepangwa kuchezwa nchini Morocco Mei 12 kabla ya kuhamia nchini Misri kwa Mchezo wa Mkondo wa Pili utakaounguruma Mei 19.