Binadamu ni neno lenye asili ya Kiarabu linalomaanisha “Mwana wa Adamu”, ana mambo sana huyu kiumbe lakini ukiachilia mbali muunganiko wa lugha ili waweze kuelewana, pia kuna tamaduni mbalimbali ambazo zinawaweka pamoja na kukuza maelewano yao, ikijumuisha mila na desturi katika kila kitu kinachowazunguka ikiwemo tabia.
Duniani kuna tamaduni zaidi ya 3800 za kipekee, zikiwemo zile za kuzoeleka na zingine si za kushangaza lakini zipo zile ambazo ukizisikia tu, basi ni lazima zitakushangaza lakini kwa jamii husika yenyewe hujivunia na kuziheshimu, kuzithamini na kuziendeleza vizazi na vizazi lakini hata hivyo zipo zitakazokushangaza.
Ukimuona Mkubwa lala chini, ni heshima.
Hii kibongobongo ni ngumu sana, lakini kwa Wanigeria ni kawaida, wao kulala kifudifudi kama kwa jamii ya wayoruba ni ishara ya heshima mbele ya wakubwa zako, hili ni kabila ambalo limechukua sehemu kubwa nchini Nigeria.
Mila ya kulala kama salamu inachukuliwa kwa ni ya uzito mkubwa hasa wakati wa kuwasalimia wazee ama watu wazima, tofauti na ilivyozoeleka hapa kwetu kwa kupiga magoti lakini kwa ndugu zetu hawa Wayoruba, kijana kulala chini kabisa na kuweka uso chini ni ishara ya utii kwa wakubwa.
Hata hivyo kuna utaratibu wa salamu hii, ipo hivi kwa Mabinti wao hupiga magoti wakati wa kusalimiana na kwa Wanaume wao hulala kifudifudi, ikiwa ni ishara ya heshima kwa wazee katika jamii na utamaduni huo ndiyo huwatofautisha Wayoruba na makabila mengine nchini Nigeria.