Scholastica Msewa – Rufiji.
Mwenge wa Uhuru 2024 umelazimika kupokea taarifa ya miradi miwili ya maendeleo iliyopo Utete makao makuu ya wilaya ya Rufiji katika Kitongoji cha Bomba, kijiji cha Nyamwage baada ya kushindwa kufika eneo la tukio kutokana na maji kufunika barabara, hali iliyopelekea Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava kutoa agizo la kuwasilishwa kwa nyaraka na picha mjongefu, ili aweze kukagua miradi hiyo.
Mbali ya msafara kukwama pia kijiko kilichokuwa kinategemewa kuvusha magari nacho kilinasa kwenye maji kufuatia utengenezaji wa barabara ambayo ingekufikisha katika miradi hiyo miwili ni kati ya nane iliyolengwa kutembelewa na kukagua katika kata ya Utete kutokana na changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Miradi hiyo, ni pamoja mradi wa barabara kiwango cha lami wenye thamani ya sh. Milioni 550 pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji kijiji cha Nyandakatundu, Utete wenye thamani ya sh. Milioni 7.9.
Awali, akisoma taarifa ya mradi wa barabara ya Utete Meneja Tarura Wilaya ya Rufiji, Hamisi Muhidini Chikaula amesema ujenzi ulianza kutekelezwa Agosti 11, 2022 na umekamilika April 10, 2023 ukigharimu kiasi cha sh. milioni 504.9 ambazo ni fedha kutoka Serikali Kuu kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani Rufiji na utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele alisema Miradi saba itazinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 757 na kukimbizwa katika umbali wa kilomita 163.5 na miradi nane itakaguliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Ametaja miradi iliyokaguliwa kuwa ni pamoja na ghala la chakula lililopo katika kijiji cha Ikwiriri Kaskazini, Bweni la wasichana shule ya Sekondari Ikwiriri, mradi wa mazingira katika Shule ya msingi Shaurimoyo, Shule ya Msingi Mgomba kijiji cha Mgomba yenye watoto wenye uhitaji maalum na kutembelea kikundi cha ushonaji Umwe Kati.