Klabu ya Manchester United ni miongoni mwa Klabu zinazotajwa kumuwania Mshambuliaji kutoka nchini Brazil na Klabu ya Barcelona ya Hispania Vitor Roque.
Gazeti la The Sun limeripoti kuwa, kutokana na kanuni za fedha ‘FFP’, FC Barcelona wanaweza kuafiki kumuuza mchezaji huyo mwishoni mwa msimu huu, na klabu itakayohitaji huduma yake italazimika kumsajili jumla na si kwa mkopo.
Gazeti hilo limeandika: “Nyota huyo wa Brazil amevutia tangu awasili Barcelona kutoka Athletico Paranaense.
“Roque mwenye umri wa miaka 19, amefunga mabao mawili kwa wababe hao wa La Liga katika mechi 13 alizocheza na anatarajiwa kuwa bora zaidi.
“Hata hivyo, anaweza kuondoka FC Barcelona kutokana na sheria za usajili.
“Hatua hiyo imezivutia klabu za Sevilla, Real Betis (Hispania), SSC Napoli (Italia), Nice (Ufaransa) pamoja na Man United (England) kuanza kuiwinda saini ya kinda huyo.
“Hata hivyo, inadaiwa kwamba Roque anataka kubaki Barcelona na atafikiria tu kuondoka kwa mkopo, japo hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.”