Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans upo kwenye mazungumzo na Kiungo Mshambuliaji kutoka Burkina Faso Stephane Aziz Ki, kwa kumsainisha mkataba mpya wa miaka miwili.

Mkataba wa kiungo huyo aliyejiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu uliopita, unatarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, huku ikielezwa kuwa Uongozi wa Klabu hiyo umeweka nguvu kubwa ili kuhakikisha anabaki klkabuni hapo.

Taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa pande zote mbili zimefikia makubaliano na kwamba kilichobaki ni Aziz Ki tu kutia saini mkataba mpya kabla ya kwenda kwao kwa mapumziko msimu huu utakapomalizika.

Mtoa habari huyo amesema wakala wa Aziz Ki ambaye ni mama yake mzazi, alikuwapo nchini kwa ajili ya kukamilisha dili lake la kuongeza mkataba na kila kitu kimeenda vizuri baada ya mchezaji huyo kukubali kusalia ndani ya kikosi cha Young Africans kwa miaka miwili mingine.

“Mbali na Aziz Ki, kuna wachezaji wengine wapo kwenye mazungumzo ya kuongezewa mkataba akiwamo Shomari (Kibwana) ambaye Azam FC wanamuhitaji. Wanaendelea kufanya mazungumzo na nyota ambao mikataba yao ipo ukingoni na wapo kwenye mipango ya Gamondi.”

“Kuhusu wachezaji wapya, wapo kwenye mazungumzo na Yusuph Kagoma wa Singida Fountain Gate FC, lakini wanazungumza na kiungo wa Simba SC Clatous (Chama) ambaye bado mambo hayako sawa,” kimeeleza chanzo hicho.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe, amekiri kuwa baadhi ya nyota wao mikataba yao ipo ukingoni na wako nao katika mazungumzo akiwamo Aziz Ki na nyota wengine ambao wapo kwenye mipango ya kocha Miguel kwa msimu ujao.

“Mkataba wa Aziz Ki unafikia ukingoni na utamalizika mwishoni mwa msimu huu, ninachokijua sasa hawezi kujiunga na timu nyingine, moja ya mikakati ya Rais wa Young Africans, Hersi (Saidi) ni kuhakikisha wachezaji wetu bora wanasaini mkataba mpya akiwamo Stephane.” amesema Kamwe

Tabora United yapigwa na kitu kizito
Makala: Hivi Waafrika ni nani aliyeturoga