Mabingwa wa Soka Tanzania bara Young Africans ni kama wameamua kujiimarisha zaidi kwa ajili ya msimu ujao, inaelezwa chini ya Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, wameanza mazungumzo na nyota wa Simba SC Kibu Denis.

Mkataba wa mchezaji huyo na Simba SC unaisha mwishoni mwa msimu huu ingawa Simba SC wanataka kumbakisha mchezaji huyo, taarifa zinasema tayari uongozi wa Young Africans umeingilia kati na kuanza mazungumzo ya kumsajili nyota huyo.

Inaelezwa Young Africans wameweka mezani ofa ya shilingi milioni 150 pamoja gari kwa mchezaji huyo wa zamani wa Mbeya City na tayari uongozi wa Young Africans upo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo, ambaye mkataba wake unafika ukingoni mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es salaam zinasema viongozi wa Young Africans wameanza mazungumzo na nyota huyo na kuweka ofa hiyo mezani lakini Kibu hajatoa tamko lolote la kukubali au kukataa ofa hiyo iliyokwa mezani na mabosi wa Young Africans.

Mtoa taarifa amesema Kibu ameingia katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa na Young Africans baada ya Kocha Miguel Gamondi kutaka kuongezewa mshambuliaji mzawa kwa lengo la kuimarisha safu hiyo ya ushambuliaji.

“Licha ya kuwekewa ofa hiyo hadi sasa Kibu hajasema lolote kuhusu kukubali au kukataa, hii inatokana na kusubiria waajiriwa wake Simba SC kuhusu ofa yao, pia Azam FC nao wameonyesha nia ya kuhitaji huduma ya nyota huyo,” amesema mtoa taarifa hizo.

Amesema Simba SC nao hawajakata tamaa ya kumbakisha nchezaji huyo kwani nao wamemwekea ofa mezani.

“Sasa hivi Kibu ndio mwenye uamuzi kuamua wapi atie saini, ana ofa mbili za uhakika lakini pia Azam FC wameonyesha nia ya kumtaka pia,” amesema mtoa habari huyo.

Ameongeza kuwa mchakato wa usajili unaendelea kwa kasi ndani ya Young Africans, baada ya viongozi na Benchi la Ufundi linaloongozwa Gamondi kukubaliana kuachana na Agustino Okrah na nafasi yake kuchukuliwa na Prince Dube.

“Kuhusu Musonda (Kennedy) kuna uwezekano mkubwa Young Africans kubadilishana na mchezaji kutoka TP Mazembe, Phillipe Kinzumbi, mazungumzo kati ya Hersi na Rais wa klabu hiyo ya  mchezaji huyo, yanaendelea nchini DR Congo,” amesema mtoa taarifa hizo

Ofisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amebainisha kuwa wapo makini sana katika usajili na wanachokifanya ni kuanza kuangalia na kufanyia kazi mapendekezo ya awali ya Benchi la Ufundi katika usajili.

“Niwaambie kuwa tutawashangaza watu kwenye usajili ujao, kwa sababu tunahitaji msimu ujao tuendelee kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa, wasubiri kuona kile viongozi wanachofanya,” amesema Kamwe

Feisal: Sishindani na yoyote Ligi Kuu
Uchakataji wa Madini: Tumieni vifaa vyenye ubora - Nesvinga