Nyota wa filamu na mchekesha mahiri nchini Idris Sultan awa sehemu ya vivutio vikubwa katika hafla ya uzinduzi wa msimu wa tatu wa tamthilia ya Bridgerton, iliyokusanya wasanii mahiri kutoka mataifa mbali mbali barani Afrika.
Onyesho hilo lililofanyika Mei 4 mwaka 2024, liliandaliwa na Netflix ambao ndio watakaohusika na urushaji wa tamthilia hiyo, ambapo msimu wa kwanza unatarajiwa kuachiwa rasmi ifikapo Mei 16 2024.
Regency Era Splendor, Into the sportlights ndio jina lililopewa onyesho hilo, ambalo lilihudhuriwa na nyota wakubwa kutoka Tanzania, (Idris), Nigeria, Kenya, Ghana, Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini, wakiongozwa na Adjoa Andoh ‘ambaye amecheza kama Lady Aga kwenye Bridgerton’ akiwa kama mgeni wa heshima.
Katika hafla hiyo muigizaji Idris aliipeperusha vyema bendera ya tanzania kama mmoja wa wageni aliyekonga nyoyo za watu wengi kutokana na muonekano wake uliopendezeshwa na mtindo wa mavazi wa kibunifu.
Kutokana na kupokea mialiko na kushirikishwa kwenye kazi za kimataifa, Sultan anaendelea kubaki kwenye orodha ya nyota wachache kutoka Tanzania wanaoendelea kujitahidi kuzichanua mbawa za sanaa ya filamu nchini ili kuipekeka kimataifa, akilishika taji la kuwa nyota wa kwanza wa kutoka Tanzania aliyepata fursa ya kuonekana kupitia Netflix akiwa mmoja wa washiriki wa filamu iitwayo Slay iliyotoka mwaka 2021.
Na baadaye mwaka 2023 alipata fursa ya kushiriki kwenye filamu nyingine iitwayo ‘Married to Work’ iliyoongozwa na muongozaji mahiri Philippe Bresson, kazi zilizomsogeza zaidi Idris kwenye soko la Afrika huku akiendelea na ubunifu na uzalishaji wa maudhui mbali mbali.
Pamoja na Idris, nyota wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na mchekeshaji na mtayarishaji Elsa Majimbo na Catherine Kamau (Kate) kutoka Kenya, nyota wa muziki wa hip hop kutoka Afrika Kusini Musa Keys aliyeambatana na nyota wengine kutoka nchini humo.