Kwa wale wakongwe wenzangu ambao tuna undugu na Wahenga, mtakuwa ama mnakumbuka au nawakumbusha kuhusu kisa hiki adhimu cha Kijana mmoja aliyeitwa Chaupele, ni simulizi ambayo ilibamba sana kama picha la ‘Sisu’ na kipindi hiko hakukuwa na luninga wala viswaswadu lakini watu waliinjoi aisee ikawa hadithi ya mjini.

Kijana aliitwa Chaupele kutokana na maradhi ya vipele vya miguuni alivyokuwa navyo, alihangaika sana na siku moja akiwa amekaa Nzi wakaanza kumsumbua kwa kutua kwenye vidonda vyake vya upele wa miguuni, alichofanya akawafanyia ‘timing’ akawachapa kwa mikono na kuua nzi saba kwa mpigo.

Ilikuwa shangwe kwake akijiona shujaa Rambo anasubiri, kiasi ikampelekea kwenda kwa fundi nguo ili amshonee kanzu iliyoandikwa “NIMEUWA SABA KWA MPIGO” hapo habari zake zikaenea na maswali kibao uraiani watu wakijiuliza ilikuwaje? na hii ilipelekea baadhi kumuogopa wakihisi ni mtu wa ‘Martial Arts’.

Kuna msemo unasema ‘Mwana kulitafuta mwana kulipata’ ee bwana wee, Nchi si ikavamiwa na mijitu mikubwa miwili ambayo ilikuwa inaishi msituni, unaambiwa hayo mijitu yaliwaua Wanajeshi wengi na kuzua hofu uraiani, na ndipo Mfalme akatangaza atampa cheo yeyote atakayewaua hao majitu lakini watu waligoma.

Hata hivyo, baadaye ‘Wadaku’ wakampenyezea habari Mfalme kuwa kuna mtu hatari sana aliwahi kuua saba kwa mpigo labda wamtafute ataokoa na hili balaa. Walichokuwa hawakijui jamaa (Chaupele), aliua nzi saba kwa mpigo na siyo watu, lakini bila kuhoji na kufanya utafiti Mfalme akaagiza aletwe mara moja.

Alikabidhiwa Mkuki na Manati, ili aende kupambana naMajitu hayo msitu mtu yapatayo mawili huko msituni, safari ikaanza na ilikuwa ni ya usiku wenye giza kufika umbali mrefu alipochoka akaamua kupanda juu ya Mti wa matunda ili apate mlo na kupumzika.

 

Ghafla ilpotimu usiku wa manane akiwa juu ya mti akasikia majitu yale yakijongea alipo na yakapumzika chini ya mti uleule kisha yakaanza kukoroma kwa usingizi fofofo, wakati yakianza kuamka taratibu akalichuma tunda moja na kuliweka kwenye manati, kisha akamlenga jicho jitu moja kwa maana macho yao yalikuwa yanang’aa kwenye mbalamwezi.

Jitu lile likampiga mwenzake ngumi na kumwambia aache uchokozi, kisha wakatulia kwa muda na ndipo Chaupele akapata nafasi ya kumlenga tena mwingine jicho, ugomvi ukazuka na majitu yale yakaanza kupigana na kuchomana visu, hadi mmoja alipokufa na mwingine akiwa hoi, kisha Chaupele akashuka juu ya Mti na kummalizia aliyebaki.

Alirudi hadi kwa Mfalme kupeleka taarifa na bada ya uthibitisho jamaa akapewa cheo cha ulinzi. Ushujaa ukatamalaki akijua alimaliza kazi lakini siku moja tena akatokea Simba mla watu, jamaa akaambiwa aende msituni amwue na akiweza atapewa Binti wa Mfalme ili awe mkewe.

Huku akiwa na hofu, Chaupele alijua mwisho wake umefika lakini alipiga moyo konde akaenda na laipofika msituni akaingia ndani ya nyumba mbovu na kuketi, mara Simba yule akaingia mlangoni, akawaza itakuwaje na atafanyaje na Simba ndo yupo mlangoni?.

Kwa akili ya haraka Chaupele aliruka dirishani akatua nje na kwa haraka akausindika mlango akamfungia yule Simba ndani, halafu akaenda kwa Mfalme na kumwambia kuwa amemkamata Simba mzima mzima, alikuwa anakunywa maji halafu akamburuta kwa mkia na kumchapa viboko mgongoni mpaka simba akatii amri, mfalme alishangaa sana.

Chaupele akaweka sumu kwenye nyama na kwenda kumrushia simba kupitia dirishani, ndipo yule Simba baada ya kula ile nyama akafa na Chaupele akaozeshwa binti wa mfalme, kitu ambacho kikaleta wivu kwa Vijana wengi ambao sasa walijipanga ili wamwue kwa minajili ya kumchukulia mke wake, kisha walikodi majambazi 28 ambao walizunguka nyumba ya Chaupele usiku wa manane kutekeleza zoezi.

Kama ujuavyo, watu hawakunyimi maneno, mke wa Chaupele alipata tetesi kwamba wamezungukwa na majambazi, akampa taarifa mumewe, na kwa vile Chaupele anafahamu wamezungukwa akili ya haraha ikamuijia akaanza kuongea kwa sauti ili majambazi yasikie.

Alisema, “Mke wangu, Nasikia tumezungukwa na majambazi 28, si unakumbuka niliuwa saba kwa mpigo, je kwenye hao 28 nitauwa saba saba ngapi?,” Mkewe akajibu “Utauwa saba nne” Chaupele akauliza tena kwahiyo nianze na saba za upande upi?…. majambazi waliposikia huo mjadala wakakimbia mana hawakujua ataanzia wapi, Chaupele na mkewe wakaishi kwa amani na mustarehe.

Ama kweli wakati umeensa wapi? zipo hadithi nyingi kama za Bulicheka, kisa cha Wagagagigikoko, Obi Mvuvi Shujaa, Mfalme Juha na hata za mtata Abunuwasi. Hakika mambo yalikuwa ‘bambam’ na watu tulifurahia hebu tujenge utamaduni wa kurithisha vizazi urithi uliotukuka wa hadithi hizi zenye kutafakarisha na zenye maarifa na zenye kujenga. Alamsiki.

Serikali yabaini changamoto za Wachimbaji wadogo
Siri za Balua, Chasambi zafichuliwa