Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema kufuatia utafiti uliofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika mikoa tisa (9) nchini, Serikali imeweza kubaini maeneo manne ya changamoto zinazowakibili wachimbaji wadogo wa madini wakiwemo wa Singida Mashariki.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo hii leo Mei 10, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Nusrat Hanje kwa niaba ya Waziri wa Madini Anthony Mavunde, katika swali lake la msingi, Mhe. Nusrat Hanje alitaka kujua ni lini Serikali itawezesha Wachimbaji Wadogo wa Madini Singida Mashariki.

‘’Mheshimiwa Spika, changamoto hizo ni pamoja na kutokuwa na uelewa kuhusu Sheria na Kanuni za sekta ya madini, taarifa za kijiolojia ya maeneo wanayochimba, mitaji na upatikanaji wa maeneo ya kuchimba madini,’’ amesema Dkt. Kiruswa.

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kutatua changamoto hizo kwa kutoa elimu, kuwapatia vifaa vya uchorongaji, kuwaunganisha na taasisi za kutoa mikopo na vifaa vya uchimbaji sambamba na kutenga maeneo mahsusi kwa ajili yao, na kueleza, ‘’ wachimbaji wadogo wa Singida Mashariki wako katika mpango endelevu wa Serikali wa kuwezeshwa ili waweze kufanya uchimbaji wenye tija.”

Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa, mpango huo endelevu wa kuwawezesha kufanya shughuli zao za uchimbaji kwa manufaa zaidi pia unajumuisha wachimbaji wadogo kutoka maeneo mbalimbali tofauti hapa nchini.

Akizungumzia malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Singida Gold Mine unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Gold Mining, Dkt. Kiruswa amesema kuwa tayari mgodi huo umekwishawalipa wananchi waliokuwa wakiishi eneo la mgodi, lakini kwa wale baadhi waliopo katika eneo la leseni mchakato wa kuwalipa fidia unaendelea mwaka huu.

Zanzibar, Bara kushirikiana ujenzi wa Miradi
Kujiamini, Ubunifu ni njia sahihi za mafanikio