Wakati Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda, akiipongeza Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, amesema kwa sasa yupo katika darasa la kuwafunda nyota wake, Freddy Michael, Edwin Balua na Ladack Chasambi, kwa lengo la kusaidia timu kupata matokeo chanya.
Freddy alikosa mabao ya wazi katika mechi dhidi ya Kagera Sugar huku Balua na Chasambi, wao wanatakiwa kucheza kitimu zaidi na kuacha ubinafsi.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Mgunda amesema yeye kama mwanamichezo, anaipongeza Young Africans kwa sababu imeshatangazwa kuwa mabingwa.
“Nchi yote imeshajua wamekuwa mabingwa, yote kwa yote hii ni michezo, tuwapongeze, wameshatangaza ubingwa, ni jambo jema, nadhani mbio za ubingwa zimeshaisha, sasa tuendelee na mbio zetu na tuombeane heri,” amesema Mgunda.
Kuhusu mechi dhidi ya Kagera Sugar, Mgunda amesema mashabiki wengi walionyesha kutoridhishwa na Freddy ambaye alikosa mabao mawili ya wazi, lakini pia walionekana kuwakosoa nyota vijana, Chasarnbi na Balua kwa tabia ya ubinafsi iliyopelekea kuikosesha timu kufunga mabao rahisi katika mchezo huo.
Kocha huyo amesema suala hilo tayari ameshaanza kulifanyia kazi kwa kuwaandalia mafunzo maalumu na anaamini hayatajirudia.
“Kwa upande wa Freddy nimekaa na mchezaji mwenyewe, nimemweleza nini cha kufanya siku nyingine ukija mpira kama ule usifanye hivi, unatakiwa kufanya hivi. Sisi kama walimu ambao tumecheza soka tunajua sababu ni nini, na tunataka kumrekebisha ili baadae tujue tatizo ni yeye mwenyewe, au huwa hajiweki sehemu nzuri.
“Lazima tuamini hakuna Mshambuliaji ambaye ananuia kutofunga, inapotokea huwa na sababu, ama za yeye mwenyewe, au anapofika langoni anakuwa bado hajajiandaa kumaliza kazi ya kuuweka mpira wavuni, hiyo sisi ndiyo kazi yetu, kuyapunguza au kuyaondoa makosa kama hayo,” amesema Mgunda.
Kuhusu Balua na Chasambi, amesema amekaa nao na kuwaeleza namna ya kufunga bao gumu na jepesi, huku akiwataka kutolazimisha kufunga sehemu ambayo ni ngumu.
“Balua alipiga mpira kwenye eneo ambalo kipa yupo, Chasambi pamoja na kufunga, ile shauku ya kutaka kufunga zaidi ndiyo maana amefanya vile,” amesema kocha huyo