Kuwa na akili ni kuwa na uwezo wa kupata ufumbuzi wa matatizo au kutoa msaada wa jinsi ya kufanya au kufanikisha jambo fulani na ili uitwe una akili, basi linapotokea tatizo inatakiwa utoe njia ya kulitatua kwa lengo la kupata ufumbuzi maana sio kila akili inafaa, au sio kila akili ni nzuri.
Kuna aina nyingi za akili, lakini tunachokitaka ni kuzitambua akili bora zaidi ya nyingine kwani ukiwa na akili ambayo wakati wa tatizo inashindwa kutoa ufumbuzi, basi hapo unakuwa umepungukiwa.
Tuchukulie mfano unatumia kikokotoo, unaandika mbili mara mbili inaleta jibu 10, je kuna maana ya kuwa na kikokotoo kama hicho? ni kweli kilifanya kazi maana kilijumlisha hiyo inatosha kuona kuna jambo limefanyika lakini vipi kuhusu jibu lisilo sahihi.
Watani zangu Wasukuma husema akili ni “problems solver” wakimaanisha upo umuhimu wa kupima ubora wa akili katika uwezo wake wa kutoa ufumbuzi wa tatizo.
Hata hivyo, neno akili tunaweza kuliita jina lingine ambalo ni “Utambuzi” kwani utambuzi, ni hali ya kugundua au kujua baada ya kutokujua, au kufichua kile kilicho fichika.
Akili lazima iweze kutambua vitu ambavyo kwa kawaida ni vigumu kuvijua au kuvipatia utatuzi na ieleweke kuwa na akili sio tu kuhusu kuwa na uwezo mkubwa wa akili kufikiri bali namna unavyoshughulikia mambo yanayoleta majawabu chanya.
Hata hivyo, Binadamu hutofautiana katika uwezo wa kufikiri na kutatua mambo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na akili yenyewe, msongo wa mawazo, akili ya kusahau, kuijaza mambo mengi, kazi afanyayo mtu au umbile kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Zipo ishara mbalimbali kuhusu akili zenye uwezo wa kubaini na kutatua mambo mbalimbali, lakini hapa nakujuza kuhusu mambo matano tu, ya kumtambua mtu mwenye uwezo wa kufikiri kwa hali ya juu.
1. Kupima hoja: Mtu mwenye uwezo wa kupima hoja, mwenye kumbukumbu na mtatuzi wa matatizo ni mmoja wapo kati ya watu wenye akili na uwezo wa juu wa kufikiri.
2. Mdadisi: Mara nyingi watu wenye akili nyingi wana hamu kubwa ya kujifunza na kuchunguza mambo, ili waweze kujifunza jambo jipya.
3. Mwenye shaka: Namaanisha shaka za kisayansi, yani watu wenye akili huwa wanahoji kila kitu kwa umakini wakilenga kupata uhalisia wa mambo na kiundani, hawakubali kitu kirahisi.
4. Wachunguzi: Jambo hili ni moja ya ujuzi muhimu wa watu wenye akili nyingi, ni vyema kulichunguza jambo lolote kwa umakini badala ya kukurupuka, penda kutilia mashaka ili ujiridhishe na uhalisia wa kitu.
5. Hisia za juu: Watu kama hao wana ufahamu bora wa hisia na maamuzi ya kuungana na wengine, mara nyingi husoma nyakati na hata kumsoma mtu kisaikolojia na wakapata ukweli wa jambo bila hata kuuliza.
Kwa wasiofahamu, akili ni kipawa kinachowezesha kufikiri, kuelewa, kuwasiliana, kujifunza, kupanga na hata kutatua matatizo, pia ni ufahamu uliomo katika ubongo hasa wa binadamu unao muwezeshakutofautisha jambo jema na baya na ili kumuongoza katika kufanya maamuzi kwa hiari yake.