Waajiri wote wa sekta binafsi ambao wanakata michango ya Wafanyakazi wao bila kuiwasilisha katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), hawatavumiliwa na Serikali kwani hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria na linawanyima haki Wafanyakazi ambao wanashindwa kulipwa mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu.
Kauli hiyo, imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za NSSF, Dar es Salaam.
Amewataka waajiri wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani watakaobainika hawatabaki salama na kuwa kumkata mfanyakazi fedha bila ya kuiwasilisha katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kunamletea usumbufu anapostaafu au ajira yake inapofikia ukomo kwa kushindwa kulipwa madai yao mbalimbali kwa wakati.
Amesema, baadhi ya waajiri wanawasilisha kwenye Mifuko asilimia kumi ya mwajiriwa tu, lakini ule mchango wake wa asilimia kumi hauwasilishi jambo ambalo ni kinyume cha sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo inamtaka mwajiri kumkata mfanyakazi asilimia zote ishirini ambayo ni ya kisheria.
Ndejembi amesema baadhi ya kero za wastaafu hususan za kusubiria mafao yao kwa muda mrefu zinasababishwa na waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati hivyo kupelekea adha kubwa kwa wastaafu na kudhani Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ndio inayowazungusha jambo ambalo muda mwingine sio kweli.
“Sasa tutakuwa wakali sana kwa waajiri wote ambao hawawasilishi michango kwa wakati kwani suala hilo ni kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii kuhakikisha kuwa waajiri wanawasilisha michango yao kwa wakati na hivyo tutasimamia jambo hili kwa ukali,” amesema Ndejembi.
Aidha, amesema ameridhishwa na namna ambavyo NSSF imekuwa ikifanya vizuri ambapo ukuaji wa Mfuko umekua zaidi kuanzia kipindi ambacho Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwezi Machi 2021, thamani ya NSSF ilikuwa trilioni 4.8 lakini ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita thamani imefikia trilioni 8.1.
“Huo ni ukuaji wa hali ya juu na hii inaonesha mafanikio makubwa ya Serikali ya awamu ya sita na mafanikio ya utendaji mzuri ya Mfuko inayofanywa na Bodi ya Wadhamini, Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wa NSSF,” amesema Mhe. Ndejembi.
Amesema pamoja na mafanikio hayo lakini kuna mambo ya msingi tunataka tuyaone yakitokea ikiwemo kuongeza nguvu ya huduma kwa mteja ambaye ni Mtanzania anayechangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwa anahudumiwa kwa wakati na changamoto zao zinaendelea kupokelewa na kufanyiwa kazi.
Hata hivyo amesema NSSF katika kuendelea kuboresha huduma zake imejenga mifumo ya TEHAMA katika kuhakikisha mwanachama anapata huduma kwa haraka zaidi.
Kuhusu uwekezaji, Ndejembi amesema fedha za Watanzania ambazo zipo kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii atahakikisha zinawekezwa vizuri na kwa uadilifu kwenye miradi itakayoleta matokeo chanya na kurejesha fedha za wanachama ili kulipa mafao kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mkuu, Mshomba amemshukuru Waziri kwa kufanya ziara ya kikazi na kumuahidi kuwa yote aliyoelekeza na kuyawekea msisitizo watahakikisha wanayatekeleza.
Amesema, NSSF inaendelea kuweka mkazo katika uboreshaji wa huduma kwa wateja na jambo hilo lipo katika Mpango Mkakati wa Mfuko, ambapo kwa sasa wameelekeza nguvu kwenye matumizi ya TEHAMA.
Mshomba ameongeza kuwa wataendelea kufanya uwekezaji wenye tija kwa kufuata miongozo ya Bodi ya Wadhamini, Benki Kuu ya Tanzania na Ofisi ya Waziri Mkuu na amewaahidi wanachama kuwa dhamira ya NSSF ni kuhakikisha inakua kadiri ambavyo matarajio ya Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuwafikia wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.