Wekundu wa msimbazi Simba kesho Ijumaa (Mei 17) watakuwa wageni wa Dodoma Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara Uwanja wa Jamhuri, Dodoma leo.
Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania wanapambana kumaliza nafasi ya pili na hivyo kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Wakiwa na pointi 57 kwenye michezo 26 waliyocheza wekundu hao wa Msimbazi kama watashinda mechi zao zote zilizosalia watafikisha pointi 69 na kushika nafasi hiyo ya pili inayoshindaniwa pia na timu ya Azam yenye pointi 60 lakini wakicheza mchezo mmoja zaidi.
Simba SC ambayo sasa inanolewa na Juma Mgunda akikaimu nafasi hiyo kwa muda baada ya aliyekuwa Kodha Mkuu wa klabu hiyo, Abdelhak Benchikha kuondoka, ililazimishwa sare ya bao 1-l na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Kagera kwenye mchezo uliopita.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba SC kwa Dodoma Jiji wenyewe wataingia kwenye mchezo huo kujaribu kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo kwani inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 30 katika mechi 26 ilizocheza.
Ushindi kwenye mchezo wa kesho Ijumaa (Mei 17) utaifanya kupanda mpaka nafasi ya saba na kuishusha Ihefu yenye pointi 32 katika michezo 27 iliyocheza.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda akizungumzia mchezo huo amesema wataingia kwa lengo la kusaka ushindi kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao.
“Simba ni timu kubwa na inachostahili ni kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika sio michuano mingine, tunaupa uzito mkubwa mchezo huu, tukiweka malengo ya kupata nafasi ya kushiriki michuano hii” amesema Mgunda
Huku kwa upande wake Francis Baraza akisema bado hawako kwenye nafasi nzuri na wanaupa umuhimu mkubwa mchezo huo ili kuhakikisha wanashinda na kukaa sehemu nzuri kwenye ligi.
Tayari kikosi cha Simba SC kimewasili mjini Dodoma mapema leo Alhamis (Mei 16) tayari kwa mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.