Shirika la Posta Nchini, limepanga Kuanzisha matumizi ya magari ya umeme na kubadilisha magari yanayotumia mafuta, ili kupunguza gharama za uendeshaji katika mwaka wa 2024/25.
Hayo yamebainishwa Bungeni Jijini Dodoma hii leo Mei 16, 2024 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 .
Amesema, mpaka kufikia 2025 wataanzisha kituo cha kudhibiti na kusimamia usafirishaji (logistics main and backup control center), kuboresha kituo cha mawasiliano kwa wateja wa ndani na nje (customer call center), kutengeneza na kutumia programu ya kufuatilia mauzo (sales tracking application) kwa ajili ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato na Kutengeneza na kutumia Mfumo wa Mipango ya Rasilimali za Kampuni.
“Vilevile Kutekeleza mradi wa kujenga kituo cha kikanda kitakachojumuisha maghala maalum ya kuhifadhi bidhaa, huduma ya ugomboaji na ushuru wa forodha ili kuwezesha biashara mtandao. Lakini Kuimarisha uendeshaji wa biashara ya kusafirisha sampuli yenye tija kwa kushirikiana na wadau nchi nzima na Kutengeneza na kutekeleza mfumo wa Posta Cash e-Wallet ambao unawawezesha mawakala kuweka na kutuma fedha,” amesema Nape.
Hata hivyo, amesema Serikali imeendelea kuimarisha Sekta ya habari nchini ambapo vituo vya kurusha matangazo ya runinga vimeongezeka kutoka vituo 65 mwaka 2023 hadi vituo 68 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.6 na Cable Television zimeongezeka kutoka 57 Aprili, 2023 hadi 60 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 5.3.
Nape ameongeza kuwa, “ vituo vya kurusha matangazo ya redio vimeongezeka kutoka vituo 215 mwaka 2023 hadi vituo 231 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 7.4 na magazeti yameongezeka kutoka 321 Aprili, 2023 hadi 351 Aprili, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 9.3 na Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za utangazaji hasa maudhui mtandaoni ambayo pia yamechangia kuongeza ajira kwa vijana.”