Baada ya kumkosa katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 2024, mwaka huu, Klabu ya Simba imeanza tena mchakato wa kusaka huduma ya winga na kiungo mshambuliaji wa Ihefu, raia wa Togo, Marouf Tchakei.
Simba SC imepania kwa kiasi kikubwa kufumua kikosi chake na kutengeneza timu mpya yenye ushindani kwa ajili ya msimu jao wa mashindano, inapiga hodi kwa kiungo huyo ambaye anacheza namba moja na Clatous Chama.
Habari kutoka ndani ya Simba SC zinasema huenda safari hii wanaweza nyota huyo kirahisi kutokana na kilichoelezwa pia nyota huyo yuko tayari kupata changamoto mpya lakini bado anabanwa na mkataba wake.
Chanzo kingine kutoka Ihefu kimesema bado ana mkataba, hivyo kama Simba SC inamhitaji italazimika kufanya mazungumzo.
“Tulimhitaji dirisha dogo la usajili, lakini ilishindikana, klabu yake iliweka ngumu lakini mwenyewe alikuwa radhi kujiunga na timu yetu, akatuambia tusubiri msimu uishe atakuwa huru, sisi tunasimamia pale pale, lakini kama itakuwa vinginevyo basi tutaangalia itakavyokuwa lakini ni lazima tumng’oe, tumejidhihirisha ni mchezaji mzuri na atatusaidia sana, ameshaifahamu Ligi ya Tanzania na ameizoea,” ameongeza mtoa taarifa hizi.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa Ihefu ilimwongezea mkataba mpya Januari 24, mwaka huu baada ya uhamisho wake wa kujiunga na Wekundu wa Msimbazi kushindikana, hivyo waajiri wake wakaamua kumbana ili asiondoke bure baada ya msimu huu kumalizika.
“Tunajua Simba SC wanamhitaji, na wamezungumza naye na yeye anahitaji kwenda huko, tulichofanya ni kumwongeza mkataba ili asiondoke bure, angalau na sisi tuambulie chochote.” kimesema chanzo kutoka Ihefu.
Mchezaji huyo alijiunga na Singida Fountain Gate mwanzoni mwa msimu akitokea AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRO) kabla kuhamishwa na kupelekwa Ihefu, amekuwa katika kiwango cha hali ya juu na mwenye mchango kwa timu yake. Nyota huyo amefunga mabao tisa msimu huu akiwa na timu zote mbili.
Wakati huo tetesi zinasema Simba SC ipo katika hatua za mwisho za kumalizana na mchambuzi wa video na viwango, Alexander Kerveillant kutoka Al Nassry ya Saudi Arabia kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Mchambuzi huyo raia wa Ufaransa anatajwa kurithi mikoba ya Culvin Mavunga ambaye amekuwa na kikosi hicho kwa muda mrefu sasa.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema hiki ni kipindi cha tetesi za usajili, na haizuiliki, lakini ukweli na kila kitu kitafahamika pale Ligi Kuu Tanzania Bara itakapomalizika.
“Siku zote huwezi kuzuia tetesi za usajili, ila sisi ni kweli tutasajili, tena usajili mkubwa tu, nani tutamsajili, ni kiasi cha kusubiri, Simba SC tumekuwa na utaratibu wetu wa kumtangaza kila anayekuja katika klabu yetu,” amesema Ahmed