Kiungo kutoka nchini Hispania Rodrigo Hernández Cascante ‘Rodri’ amefichua wapi Arsenal walipokosea katika mbio za kuwania Ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu wa 2023/24.

Arsenal iliyokuwa na Kikosi Bora msimu wa 2023/24 ilionesha kupambana katika mbio za ubingwa hadi kwenye michezo ya mwisho iliyopigwa jana Jumapili (Mei 19), huku ikishinda 2-1 dhidi ya Everton na Man City ikiifunga West Hama United 3-1.

Rodri mwenye umri wa miaka 27 amesema kujipanga na dhamira njema ya kutaka kuwa mabingwa, vimewapa nafasi ya kutetea taji la England kwa mara ya nne mfululizo, lakini imekuwa tofauti kwa Arsenal.

Kiungo huyo amesema Arsenal walikosea kwenye mchezo uliowakutanisha na Man City kwenye Uwanja wa Etihad, ambapo amekiri aliwaona wapinzani wao wakicheza kwa dhumuni la kusaka sare badala ya kusaka ushindi, ambapo hali hiyo imeshindwa kuwapa furaha mwishoni mwa msimu.

“Mojawapo ya mechi hizo ni ile ya sare tasa katika uwanja wa Etihad mwishoni mwa mwezi Machi ambayo ilishuhudiwa Arsenal wakiwa na asilimia 27 pekee ya kumiliki mpira huku wakitunyima ushindi.

“Kwa hakika Arsenal walistahili kutwaa Ubingwa kwa sababu walikuwa na kikosi imara, ila tukubali walianza kukosea kwenye mchezo waliocheza hapa dhidi yetu.

“Walipofika hapa walitukabili vilivyo, lakini niliona dhumuni lao lilikuwa ni kutafuta sare badala ya kushinda, nilipoona hilo nilibaini hawa hawataweza kufikia lengo la kuwa mabingwa msimu huu.” amesema Rodri

Man City imekuwa klabu ya kwanza kutwaa Ubingwa wa Ligi ya England manne mfululizo, akivunja rekodi ya majirani zao Man Utd.

Man City watajaribu kutwaa taji lingine msimu huu 2023/24, mwishoni mwa juma hili watakapovaana na Man Utd kwenye mchezo wa Fainali Kombe la FA.

Mzee ahofia Ziwa Victoria kuumeza Mkoa wa Kagera
Aziz Ki, Fei Toto wanasakwa Msimbazi