Kutokana na Wananchi wengi kukumbana na changamoto mbalimbali za kimikataba, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya Kaskazini – TIRA, Bahati Ogolla amewataka Wadau wa Sekta ya Madini kusoma na kuielewa mikataba mbalimbali wanayopewa katika makubaliano, kabla ya kuisaini hasa katika taasisi za Bima.
Ogolla ameyasema hayo jijini Arusha hii leo Mei 23, 2024 katika Jukwaa la Tatu la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, ambalo hufanyika kila mwaka, likilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini ili kujadili na kufanya tathmini ya ushirikishwaji wa Watanzania katika mnyororo wa sekta hiyo.
Amesema, “someni mikataba vizuri kama huelewi tumia wanasheria au njoo TIRA kwa msaada zaidi, msiingie mikataba bila kujua faida na hasara, kabla ya kuisaini ni vyema kushirikisha baadhi ya watu, ili kushauriana na kuepuka matatizo na maumivu yatakayojitokeza baadaye.
Katika jukwaa hilo, TIRA imetoa mapendekezo nane ya kufuatwa ili Watanzania waweze kunufaika na huduma za BIMA, ikiwemo Wananchi kuwekewa kinga dhidi ya vihatarishi mbalimbali, kulipa ada za bima inavyotakiwa na kutambua haki na wajibu wao kwenye mikataba wa bima.
Mapendekezo mengine ni kuhakikisha wanatambua kanuni na taratibu za bima ikiwemo ulipaji wa ada ya bima, uaminifu uliotukuka, uhusiano wa umiliki wa mali na mkatabima kurejeshwa kwenye hali iliyokuwepo kabla ya janga kutokea, huku akiitaka jamii kushirikiana na mamlaka kufichua vitendo vya udanganyifu kwenye biashara ya bima, akitolea mfano madai yasiyokuwa halali.