Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wazazi na Walezi kufuatilie mienendo ya watoto wao waendapo shuleni ikiwemo na mahudhurio na masomo yao ya darasani na kwamba Serikali inaendelea kuimarisha mahudhurio ya Wanafunzi, hali itakayosaidia kuimarisha uwezo wao kitaaluma na maadili kiujumla.
Majaliwa metoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Mei 23, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda ambaye alihoji Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanafunzi wanaoanza masomo wanamaliza wote shule ukiacha wale ambao hufariki dunia.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema, “Serikali inaendelea kuimarisha mahudhurio ya watoto shuleni kwa kuzungumza na wazazi ili kuhakikisha kila mzazi anasimamia mahudhurio ya mtoto wake, kwenda shule, kuingia darasani, lakini anaporudi nyumbani, mzazi afuatilie mwenendo wa masomo ya mtoto huyo, ili ajiridhishe kama kweli mtoto alikwenda shuleni.”
Kuhusu shule za sekondari, Waziri Mkuu amesema wanaimarishwa ujenzi wa mabweni na hosteli kwa ajili ya Wanafunzi wa kike na wa kiume, ili wasome, walale na wacheze palepale na kwamba usimamizi wa maadili yao uweze kuimarika kwani tayari maelekezo yalikwishatolewa kwenye Halmashauri zote za Wilaya.
“Pia tumeimarisha taasisi yetu ya Uthibiti Ubora ambayo moja ya majukumu yake ni kuhoji idadi ya wanafunzi waliosajiliwa, waliopo darasani na wanatakiwa wahoji ni kwa nini wengine hawapo kulingana na usajili uliopo, tunaamini kupitia hatua hizi, utoro utapungua na tutaanza kuona wanafunzi waliosajiliwa wanafikia asilimia 95 hadi 98 ya wanaomaliza,” amesema Waziri Mkuu.