Maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani yamefanyika hii leo Mei 23, 2024 na kuhudhuriwa na Waandishi wa Habari, Wadau mbalimbali wa Habari pamoja na wawakilishi kutoka asasi za Kiraia huko Zanzibar, huku wengi wakiendelea kupaza sauti juu ya mapunguzu ya sheria za Habari zilizopo.

Maadhimisho hayo ambayo ni muhimu katika kukuza na kuimarisha kada ya habari, pia yametoa wito maalum kwa wadau wa habari kuhusu umuhimu wa kuwa na Sera na Sheria rafiki zitakazowezesha utendaji kazi wa vyombo vya habari kuwa na ufanisi, na hapa nakuwekea baadhi ya nukuu ambazo zimewasilishwa kwa nyakati tofauti.

Masharti kisa jinsia.

“Hupaswi kumuwekea mtu masharti kutokana na jinsi yake. Tufanye kazi kwa kuzingatia taaluma, tumewahi kuzungumza na Mhe. Rais kuhusu sheria hizi, na Waziri pia, nadhani inabidi tupange kuzungumza nao tena ili tuone hili linakwendaje. Haitapendeza hata kidogo tumalize mwaka huu na bado hatujapata mabadiliko ya sheria za habari.” Mkurugenzi – TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa.

Uhuru wa Mwandishi.

“Kauli mbiu yetu imegusa kuhusu sera na sheria, na hii tumeitumia makusudi ili tukiwa na sheria nzuri za habari ndipo waandishi wa habari watapata uwezo wa kuandika vizuri masuala ya mazingira kwa uhuru.” Mwenyekiti – Zanzibar Press Club, Abdalla Mfaume.

Maadili ya Kitaaluma.

“Waandishi wa habari tufanye kazi Kwa kuzingatia maadili ya taaluma yetu kwa kuhakikisha vyanzo vya habari vimekamilika. Kwa sasa sheria ya habari ipo kwa mwanasheria mkuu, na tunaitegemea itakwenda baraza la wawakilishi kama mswada na tunawaomba walioko kule waichangie vizuri ili iweze kupita na tupate sheria mpya.” Katibu Mtendaji, Tume ya Utangazaji Zanzibar, Suleiman Salim.

Mabadiliko ya Kiuchumi.

“Kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika vyombo vya habari ni kufikiria kwanza namna gani tunaendana na kasi ya mageuzi ya masuala ya kiteknolojia.” Katibu Mtendaji, Baraza la Habari Nchini – MCT, Ernest Sungura.

Ukweli katika utendaji.

“Waandishi wa habari katika kazi zetu tukumbuke kusema ukweli kwa kuzingatia maadili ya fani ya uandishi wa habari.” mwandishi wa Habari Mwandamiz Zanzibar, Jabir Idrissa.

Sera na Sheria bora.

“Vyombo vya Habari ni washirika wa maendeleo, hivyo kuwa na sera na sheria bora itawawezesha waandishi wa habari kuwa na mazingira rafikikatika kutekeleza majukumu yao,” mwandishi wa Habari mkongwe Zanzibar, Salim Said Salim.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya Hbari hapo jana, Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ,  Dkt, Mzuri Issa alieleza kuwa suala la kuwa na sheria mpya na nzuri ya habari, limekuwa katika mchakato na hatua mbali mbali zimechukuliwa katika kukusanya maoni ya wadau, ukishirikisha fikra na maoni tofauti ambapo masuala ya jinsia na vyombo vya Habari yatakuwa na nafasi ya kipekee.

Waandishi wawili jela kwa kutoa maoni ya uchochezi
Majaliwa: Wazazi, Walezi fuatilieni mienendo ya Watoto Shuleni