Swaum Katambo – Katavi.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani Katavi, imekamata kilogramu 110 za bangi na kuteketeza ekari tatu za mashamba ya bangi.

Hayo yameelezwa na Afisa Sheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Denastus Mnyika ambaye amesema katika tukio hilo, watuhumiwa wawili wamekamatwa kwa kuhusika na usafirishaji wa kiasi hicho cha dawa za kulevya zilizokuwa zimewekwa ndani ya mifuko ya sandarusi na watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

Amesema, ukamataji huo ulifanyika kufuatia operesheni iliyofanyika kuanzia Mei 17 – 23, 2024 katika Kijiji cha Kafisha, kilichopo Kata ya Ikola, Tarafa ya Karema, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanapambana kwa pamoja kutokomeza biashara hiyo, ili kuokoa kizazi cha sasa na baadae dhidi ya madhara yatokanayo na madawa ya kulevya.

Aidha, amewaka Wananchi wa Mkoa wa Katavi na Watanzania kwa ujumla, kuachana na biashara na uzalishaji bangi na badala yake wajikite katika kufanya shughuli zingine halali za kiuchumi.

Watoto waliozaliwa kambi ya waathiriwa wa mafuriko wafikia tisa
Inonga aukana mkataba Simba SC