Hatimaye Klabu ya AC Milan imethibitisha itaachana na Kocha Stefano Pioli aliyedumu klabuni San Siro kwa miaka mitano, itakapofika mwishoni mwa msimu huu 2023/24.
Pioli mwenye umri wa miaka 58 ataondoka klabuni hapo huku akiacha kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa Ligi Kuu ya Italia Serie A dhidi ya Torino iliyochomoza na ushindi wa 3-1 mwishoni mwa juma lililopita.
Matokeo hayo yameendelea kuwa mabaya kwa miamba hiyo ya mjini Milan, kwani imepata ushindi mara moja pekee katika michezo minane iliyopita kwenye michuano yote, ikipoteza mara nne.
Taarifa iliyothibitisha kuondoka kwa Pioli imeeleza: “AC Milan na Stefano Pioli wamefikia makubaliano ya kuvunja mkataba, Kocha ataondoka baada ya kumalizika kwa msimu huu, Tunashukuru kwa kufanya kazi na Pioli ambaye alijiunga nasi Oktoba 2019.
“AC Milan inatoa shukrani za dhati kwa Stefano Pioli na wafanyakazi wake wote kwa kukiongoza kikosi cha kwanza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kutwaa taji la Ligi lisilosahaulika na kuanzisha tena uwepo thabiti wa AC Milan katika michuano mikubwa Barani Ulaya.
“Ustadi wa Stefano na mguso wa kibinadamu umechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kikosi chetu, ikijumuisha maadili ya msingi ya klabu tangu siku ya kwanza alipoanza kufanya kazi hapa.
Pioli amesaliwa na mchezo mmoja wa Ligi Kuu ya Italia Serie A, ingawa Rossoneri watamaliza katika nafasi ya pili bila kujali matokeo ya mpambano wao dhidi ya Salernitana ambayo tayari imeshashuka daraja.