Uongozi wa Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans, umesema unapambana kumshawishi Kiungo kutoka nchini Burkina Faso Stephanie Aziz Ki, ili asaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema Young Africans imefanya mazungumzo na nyota huyo lakini ameshindwa kukubali kusaini mkataba mpya kutokana na ofa mbalimbali alizonazo.

Taarifa hizo zimeelendea kueleza kuwa mchezaji huyo ambaye kwa sasa anaongoza katika mbio za ufungaji bora Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2023/24, anasubiri kufanya uamuzi mwingine mapema mwezi ujao.

“Aziz Ki akiwa na wakala wake (mama yake), wamefanya mazungumzo vizuri na Young Africans, lakini akawaambia wasubiri, atasaini siku nyingine, aliondoka na mkataba huo na kuahidi atausaini,” kimesema chanzo cha taarifa kutoka Young Africans.

Kimeongeza licha ya Rais wa Young Africans, Hersi Said, kuongoza kikao cha mazungumzo, Aziz Ki, alionekana kushikilia uamuzi wake wa kuhitaji muda ili kukamilisha mchakato huo.

“Uongozi tayari umempa mkataba mpya, lakini bado hajausaini, Aziz Ki anaonekana kuvutiwa zaidi na ofa kutoka Afrika Kusini kwa sababu kuna timu inamtaka, kuna uwezekano akaondoka,” kimeendelea kusema chanzo hicho

Kimeongeza pia taarifa za nyota huyo kutakiwa na timu moja ya hapa nchini si kweli na hizo ni propaganda za usajili.

“Ofa ambayo Young Africans wamempa si rahisi kwa Aziz Ki aiache, halafu asaini klabu ya hapa nchini, anachelewa kusaini kwa sababu ya ofa za nje ya nchi alizonazo, hakuna klabu ya ndani ambayo anaweza kwenda huko na kuacha ofa yetu,” kimeongeza

Msemaji wa Young Africans, Ali Kamwe, amekiri  mchezaji huyo hajasaini mkataba mpya kwa sababu bado wapo katika mazungumzo.

“Niwatoe hofu mashabiki na wanachama wa Young Africans, wachezaji wote ambao bado tunawahitaji tutabaki nao msimu ujao, na hata kama kuna mchezaji ambaye tunamhitaji na akataka kuondoka hakuna timu ya hapa ndani inaweza kumchukua, labda ataenda nje ya nchi,” amesema Kamwe

Ametamba mwakani wanahitaji pia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Stefano Pioli, AC Milan ndo basi tena!
Wivu: Ngosha matatani kwa mauwaji ya mpenzi wake