Swaum Katambo – Tanganyika.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amewataka maofisa wa Serikali wilayani humo kuheshimu fedha za kodi zinazolipwa na wananchi, ili ziweze kufanya kazi za maendeleo yaliyokusudiwa na kuendelea kuwapa morali walipakodi.

Wito huo ameutoa katika kikao cha Kamati ya Ushauri wa Kodi ya Wilaya ya Tanganyika ambapo yeye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo huku akiipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA, Wilayani humo kwa kufikia asilimia 109 ya ukusanyaji wa mapato kiwilaya kwa kipindi cha miezi 10 kuanzia julai 2023 mpaka aprili 2024.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu.

Kwa upande wake Meneja msaidizi wa TRA Mkoa wa Katavi, Bernward Peter ameshukuru ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka Serikalini na walipakodi kwa ujumla kwani ndio chachu ya kufikia malengo ya ukusanyaji wa kodi kwa kipindi cha miezi 10 pekee.

Amesema, kwa mwaka wa fedha 2023/24 Wilaya ya Tanganyika ilipangiwa kukusanya kiasi cha sh 243,540,000/- hivyo Wilaya iliweza kufanikiwa kukusanya 264,943,000/- sawa na asilimia 109 ya utendaji kazi, ambayo imetokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo ajira, mapato ya biashara pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji.

Kikao cha Kamati ya Ushauri wa Kodi ya Wilaya ya Tanganyika.

Aidha,amewahamasisha Wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa manufaa ya taifa, pia kwa walipakodi wenye vigezo kutoa risiti za kielektroniki na wanunuzi pia kudai tisiti pindi wanunuapo bidhaa lengo kuu ni kupata takwimu sahihi za Serikali ambazo zinasaidia katika ukadiriaji na ukusanyaji wa mapato.

Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Hamad Mapengo amewataka TRA na maofisa biashara kuzidi kushirikiana na kuendelea kutoa elimu katika suala zima la kukusanya kodi ili kwa pamoja waharakishe kuwaletea wananchi maendeleo.

Rais Hussein Mwinyi aishukuru CAF
Stefano Pioli, AC Milan ndo basi tena!