Ukiitazama hali ya ulimwengu wa leo, unaweza kushangaa au kufurahia kwa kufikiri kwamba baadhi ya Watawala watangulizi hawakuwa makini au walikuwa mashujaa au unaweza enda mbali zaidi ukawalaumu au kuwapongeza, kutokana na vile unavyoiweka tafsiri yako katika kutazama mambo ya kale.
Hali hii siyo jambo jipya kwani tayari wengi waliotangulia nao walishangaa au kufurahia kama wewe kutokana na hisia zao, mfano kuna watu wamekuwa wakiwavumilia watawala wao ambao walipoteza umakini na kufanya mambo yasiyofaa ama ya kupendeza yaliyoacha historia, kwani baadhi yao walichekesha, wengine wakaogopwa kwa ukatili wao.
Hapa nakuletea matukio machache ambayo wewe nawe utatoa tafsiri yako kulingana na kile kilichoandikwa na Wazee wetu hawa wakongwe walioacha alama katika maisha ya Dunia kutokana na haiba yao ya uongozi na mapokeo ya wale waliowaongoza, najua hukuwepo lakini utajifunza kitu.
1. Qin Shi Huang akichunguza kifo.
Qin Shi Huang alikuwa mtawala ambaye aliamini mambo yake yeye mwenyewe. Aliingia madarakani kama mfalme wa kwanza wa China iliyoungana katika karne ya 3 KK, ambapo mara tu alipopata mamlaka, alihangaikia sana kwani alikuwa na maadui wengi na kwa miaka mingi alikabiliana na majaribio kadhaa ya kutaka kuuawa.
Wazo la kwamba kifo ndicho pekee ambacho kingeweza kumtenganisha yeye na madaraka, kilimfanya apoteze fikra kwani alikuwa na hamu ya kupata njia ya kutokufa hivyo aliwasiliana na madaktari ambao walimwekea utaratibu mzuri wa kudumisha uhai wake.
Alishindwa masharti hapo akaanza kumeza vidonge vilivyojaa zebaki lakini dawa hizo zilikuwa na athari kwani afya yake ilidhoofika na uwezo wake wa kufikiri ulipungua hivyo ikambidi kuwaagiza wasaidizi wake kwenda kudadisi wakuu wa ‘Visiwa vya Wasiokufa’ kutafuta dawa ya kichawi ambayo ingemruhusu kuishi milele.
Na kwa kuogopa watu waovu, Qin Shi Huang alikuwa na mfumo tata wa maisha ya kujificha kwani alitengeneza mfumo wa vichuguu vilivyojengwa, ambavyo viliunganisha majumba yake yapatayo 200 ili hata atakapovamiwa basi adui asiweze kufanikiwa lengo lake kirahisi, lakini hata hivyo aliaga dunia miaka ya 210 BC akiwa na umri wa miaka 49.
Huang anakumbukwa zaidi kwa utafiti wake huo wa kutokufa, kumbukumbu yake ikisalia katika kaburi lake alilozikwa pamoja na jeshi lake la askari wa terracotta, ambao kwa pamoja walikula yamini wakikusudia kuwa jeshi lisiloweza kufa, wakiapa kumlinda mfalme wao (Qin Shi Huang), aliyedaiwa kuwa naye hawezi kufa, wakipanga kutawala milele na milele.
2. Nero alimuuwa Mama yake mzazi.
Kiukweli, unaweza kuandika orodha nzima ya watawala wenye wazimu wa Kirumi, lakini aliye na wazimu zaidi kati yao alikuwa ni Mfalme wa Himaya ya Roma – Italia, Nero Claudius Caesar Augustus Germanicus, aliyeanza utawala wake akiwa na akili timamu, lakini kadri muda ulivyoklwenda alizidi kuitumbukiza jamii katika hali ya mshangao iliyompelekea kuonekana ni kweli ana wazimu.
Alifanya mambo mengi ya kijeuri lakini Nero alikuwa na upande alioegemea na ikumbukwe kwamba wakati akitawadhwa kuwa mfalme wa Roma alikuwa na umri wa miaka kumi na saba pekee, zaidi alikulia kwa kuzoeshwa kumudu mambo ya sanaa licha ya kwamba pia alikuwa mwimbaji hodari, mwanamuziki, na mkariri wa mashairi.
Katika utamaduni wa Kirumi, waigizaji wa kitaalamu na wanamuziki walikuwa wakizungumzwa sana na kijamii, yeye akiwa ni mmoja wapo kwani alipenda zaidi kuigiza na katika utawala wake kama mfalme, aliandaa hafla na mashindano kadhaa ya kucheza hadharani.
Alifikia hata kuingia kwenye Michezo ya Olimpiki na kuwalazimisha waandaaji kujumuisha mashindano ya kisanii na matokeo hayakustaajabisha, kwani alikuwa akishinda kila tukio aliloingia kama mshiriki kwani aliogopwa ni mfalme unawezaje kumshinda mfalme kwa mfano.
Alipenda sana kuigiza na alicheza kwa muda mrefu, ili aendelee kutazamwa na pale alipohisi watu wanamsema kwa kuboreka aliwatendea visivyo, kitu kilichopeleke watazamaji waliokuja tamashani kutafuta njia za kutoroka huku wengi wakiigiza mfano Wazee wangejifanya wana pressure na Wanawake wangeigiza kuumwa ili watoroke.
Inaarifiwa kuwa Nero alikuwa na tabia ya kuua watu wake wa karibu, lakini matukio yake ya uuaji yalianzia mlangoni pake baada ya kumuuwa mama yake kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi, lakini inaonekana baada ya kifo chake Nero alianza kusumbuliwa na paranoia na hapo bila shaka umenielewa kwamba ikiwa aliweza kumuuwa mama yake mwenyewe basi ni wazi kwamba angeweza kumgeukia, mtu yeyote na kumdhuru.
Inaaminika pia kwamba, Nero aliua mke wake wa kwanza na kumuua mke wake wa pili yeye mwenyewe. Baada ya mke wake wa pili, Poppaea, kufariki, alihasiwa kijana wa kawaida aliyefanana na marehemu. Kisha akamvisha kijana huyo kama mke wake na kumuoa, hapo ndipo raia waligundua na kuthibitisha ukweli wa vitendo vyake vya uwendawazimu ingawa naye alifariki mnamo June 9, 68 AD.