Josephine Majula – Kagera.

Serikali inatarajia kuanza kutumia vikao vyake rasmi kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha, ili kupunguza migogoro inayoendelea nchini kuhusu mikopo na watu kuchukuliwa mali zao, kwa kushindwa kulipa mikopo.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Isaya Mbenje wakati alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha, ambayo ilifika Kisiwa cha Bumbire kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi, ili waweze kujikomboa kiuchumi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Isaya Mbenje, akizungumza na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha (haipo pichani), ambayo ilifika ofisini kwake kujitambulisha na kuelezea njia watakazo tumia kufikisha elimu ya huduma ndogo za fedha katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Amesema, “nitahakikisha Waratibu wa Elimu Ndogo ya Fedha ngazi ya Wilaya wanapata muda wa kutoa elimu katika vikao rasmi vya Serikali ambavyo vinawahusisha watu wengi wakiwemo Waheshimwa Madiwani na watu wote ili waweze kufikisha elimu hii kwa watu wanaowasimamia.”

Mbeje ameongeza kuwa, kupitia Madiwani ambao ni Wawakilishi wa Wananchi katika ngazi ya Kata na Vijiji wakipewa elimu ya fedha vizuri na kuelewa, itawafikia wananchi wengi katika maeneo yote kwa kuwa kila Kata na Vijijini, inawawakilishi katika mikutano rasmi ya Serikali.

Baadhi ya Wananchi wa Kisiwa cha Bumbire wakiangalia filamu yenye mada mbalimbali kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha ambayo ilitumika na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kutoa elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Kagera.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata wa Kisiwa cha Bumbire, Davis Alistedius, amesema kuwa elimu waliyoipata Wananchi wa Kisiwa chake watahakikisha wanawasimamia waweze kusajili biashara zao, ili ziweze kutambulika rasmi na Serikali na kuwawezesha kufanya kazi kwa uhuru.

Naye mkazi wa Kisiwa cha Bumbire, Anorld Rweyemamu, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuwafikia na kuwapa elimu hiyo muhimu itakayowakomboa kiuchumi kupitia mada mbalimbali walizofundishwa ikiwemo uwekezaji, mikopo na umuhimu wa kuweka akiba.

Mkazi wa Kisiwa cha Bumbire, Maka Osward akiuliza swali kuhusu njia bora ya kuwekeza kwa Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika Kisiwani humo kutoa elimu ya fedha ambapo iliwafundisha wananchi hao mada mbalimbali ikiwemo kujiwekea akiba, namna bora ya kukopa na uwekezaji.

“Elimu tuliyoipata ni nzuri ila tunaiomba Serikali iendelee kuwashawishi wawekezaji hususan Taasisi za Fedha kama benki kuja kuwekeza katika Kisiwa chetu ili kupitia Taasisi hizo tuweze kujiwekea akiba na kufanya uwekezaji kupitia ununuzi wa hisa,” alisema Rweyemamu.

Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Mary Mihigo, akiwashukuru Wananchi wa Kisiwa cha Bumbire kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha amesema itawasaidia kuwa na matumizi sahihi ya fedha kutokana na mada mbalimbali walizowafundisha ikiwemo usimamizi wa fedha binafsi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Isaya Mbenje, akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha, ambayo ipo mkoani Kagera kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha. Kutoka kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Mary Mihigo, Afisa Biashara na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Wilaya ya Muleba, Joseph Masawe, Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya na Afisa Mwandamizi Uchambuzi Masuala ya Fedha kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Gladness Mollel.

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika mikoa nane ikiwemo Kagera, Singida na Manyara ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.

Afisa Mwandamizi wa Uchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Gladness Mollel, akitoa elimu kwa Wananchi wa Kisiwa cha Bumbire kuhusu masuala ya uwekezaji wilayani Muleba mkoani Kagera.

(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Kagera)

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 29, 2024
Rasha aendeleza uibuaji wa tabasamu kwa jamii, atoa wito