Mzee Kimbwembwe kutoka Kijiji cha Somanga, ambaye Julai 30, 2020 alipata umaarufu baada ya kumkabidhi zawadi ya jogoo Rais wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ameibuka na taswira ile ile kwa kumpatia Jogoo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kumpongeza kwa jitihada za urejeshaji wa mawasiliano ya Barabara eneo la Tingi – Kipatimo na ile inayounganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.

Kimbwembwe amekabidhi Jogoo huyo, muda mchache kabla ya Waziri Bashungwa kuwasilisha bajeti yake Bungeni kwa mwaka wa Fedha wa 2024/25 hii leo Mei 29, 2024 huku akisema bado ipoa zawadi kubwa waliyomuandalia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema, “na wewe Bashungwa kwa kauli moja sisi wananchi wa Kilwa tumekuletea zawadi hii kutokana na kazi kubwa uliyoifanya kwa kurudisha mawasiliano ndani ya saa 72 kama ulivyoahidi, tunachojua ulifika pale kwa sababu ya maelekezo maalumu ya Rais wetu kipenzi Dkt Samia Suluhu Hassan, sisi wananchi wa Kilwa kuna zawadi tuliyomuandalia ambayo siwezi kuitaja leo.”

Mzee huyo amesema kilichowafurahisha wananchi, ni kitendo cha Waziri kukaa huko kwa siku tano akishughulika na urudishaji miundombinu iliyokatika kwa sababu ya mvua kubwa, jambo linaloonyesha kujali ambapo mara baada ya kupokea zawadi hiyo, Waziri Bashungwa amesema imempa nguvu na kuahidi kurudi tena katika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia hali ilivyo.

Serikali kushirikisha Sekta binafsi utekelezaji miradi ya miundombinu
Putin adaiwa kuchangia mgawanyiko EU