Walimu wenye madai ya malimbikizo ya mishahara, wametakiwa kuwasilisha vielelezo vya madai yao kwa Maafisa Elimu ili yashughulikiwe, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa anayetaka changamoto zote za walimu zitatuliwe.
Wito huo, umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde wakati wa vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri za Wilaya ya Biharamulo na Muleba.
Amesema, “Walimu kuanzia sasa wasilisheni madai yenu na viambata vyake muhimu kwa Maafisa Elimu ili wao ndio wawasilishe kwa Maafisa Utumishi kwa ajili ya kushughulikiwa, na kuongeza kuwa waziri mwenye dhamana Mhe. Mohamed Mchengerwa alishaelekeza madai yote ya walimu yashughulikiwe.”
Dkt. Msonde amesema, Maafisa Elimu watekeleze jukumu hilo kwani wapo kwa ajili ya kuwahudumia walimu hivyo ni wajibu wao kuwafuata Maafisa Utumishi Wakuu ili kushirikiana nao katika kushughulikia madai ya malimbikizo ya walimu na kuhimiza Afisa Elimu baada ya kushughulikia madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi kwa Afisa Utumishi Mkuu, anapaswa pia kuwapatia mrejesho watumishi husika ili wajue ni hatua ipi imefikiwa katika kushughulikia madai yao.
“Afisa Elimu iwapo ukienda kwa Afisa Utumishi na asikupe ushirikiano, nenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na unijulishe mimi ili tuchukue hatua stahiki kwa Afisa Utumishi huyo ambaye anakaidi maelekezo halali ya waziri mwenye dhamana Mhe. Mohamed Mchengerwa,” amesisitiza Dkt. Msonde.