Mshambuliaji na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ufaransa Kylian Mbappe amesema yupo tayari kuianika hadharani Klabu atakayoitumikia msimu ujao 2024/25.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, amewaacha njia panda mashabiki wake, ambao wanatamani kufahamu wapi atakapocheza msimu ujao, Licha ya Miamba ya Soka mjini Madrid- Hispania Real Madrid kutajwa kuwa kwenye nafasi nzuri ya kumsajili katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.
Mbappe ameweka wazi mpango wa kuitangaza Klabu atakayoitumikia msimu ujao, alipohojiwa na Kituo cha Televisheni cha CNN cha nchini Marekani, ambapo amesema muda si mrefu wataweka kila kitu hadharani.
Amesema anafahamu Mashabiki wake wana hamu ya kuifahamu klabu hiyo, lakini hawana budi kusubiri kwa kipindi kifupi kijacho, ambacho kitafumbua fumbo hilo lililodumu kwa muda mrefu.
“Klabu yangu ijayo itakuwa hadharani hivi karibuni, ni suala la muda tu. Nimefurahia sana, na ninaendelea kuwa na furaha kwa hatua nitakayopiga.
“Inabidi mashabiki wangu waendelee kusubiri kwa sababu sio siuku nyingi sana zilizosalia, kabla sijatangaza maamuzi yangu binafsi.”
Wakati wa kusaini mkataba wake mpya mwaka 2022 akiwa na Mabingwa wa Ufaransa PSG, Mbappe alieleza: “Lilikuwa swali ambalo lilienda zaidi ya kubaki PSG tu, lilikuwa Kombe la Dunia nchini Qatar, kulikuwa na mambo mengi kuhusu mimi. Ulikuwa uamuzi mkubwa, uamuzi mgumu, lakini Sijutii chochote.”
“Bila shaka katika maisha ni lazima ufanye maamuzi magumu na ndivyo nilivyofanya, lakini nikawa mfungaji bora wa muda wote wa PSG, ninajivunia hilo. Nataka kukumbuka mambo mazuri zaidi… hali rahisi na ninatamani hakuna mtu angeipitia.”
Mei 10, 2024, Mbappé alitangaza kupitia mitandao ya kijamii kwamba ataondoka Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu akisema hataongeza mkataba ndani ya Klabu hiyo, hatua ambayo iliashiria mwisho wa utumishi wake huko Parc de Princes.
Mei 12, alicheza mechi yake ya mwisho kama mchezaji wa PSG, akifunga bao la kufutia machozi dhidi ya Toulouse iliyoibuka na ushindi wa 3-1. Alitumikia PSG mchezo wake wa mwisho Mei 25, katika Fainali ya Kombe la Ufaransa ‘Coupe de France’ dhidi ya Lyon, PSG ikishinda 2-1.