Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba SC, Ismail Aden Rage wameshauri viongozi wa timu hiyo kutohangaika na kuleta Kocha mpya wa kigeni, badala yake wamuamini Kaimu Kocha Mkuu wa sasa Juma Mgunda na kumkabidhi rasmi timu hiyo kama kocha mkuu kwani anao uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa na kufikia malengo ya klabu.
Rage amesema hayo baada ya Ligi kumalizika huku Simba SC wakimaliza nafasi ya tatu na kuangukia Kombe la Shirikisho Barani Afrika ambapo hayakuwa malengo yao msimu huu.
Aidha, Rage amewapongeza Young Africans kwa kufanya vizuri kwenye ligi ya ndani kwa kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo na kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF, huku akiwashauri kufanya usajili kuboresha kikosi chao ili waweze kufanya vizuri zaidi msimu ujao na misimu mingine inayokuja.
“Simba SC imekuwa ya tatu kwenye ligi licha ya kuingia kwenye Robo Fainali mara tano kwenye michuano ya Afrika na ukiwaangalia wenzetu kama Orlando Pirates na Kaizer Chiefs hawajulikani wako wapi.”
“Niwashauri Simba SC wasipaniki wala kugombana na viongozi wao, wamsikilize kocha ambaye mimi ninamuamini kwa sababu ana taaluma kubwa kuliko kocha yoyote wa Kitanzania.”
“Simba SC waige kama wanavyofanya Afrika Magharibi wanatumia makocha wao wazawa. Rekodi ambayo Simba SC wanayo kwa kufanikiwa mwaka 1974, nikiwa mchezaji tulikwenda nusu fainali na Kocha Paul West Bivaha mwenyeji wa Iringa. Kuna King Kibaden mwaka 1993 aliifikisha Simba fainali ya kombe la washindi Afrika.”
“Kama uongozi wa Simba SC watamheshimu Mgunda ambaye ana sifa zote kama mchezaji na kocha, anaongea Kiswahili na Kingereza kwa ufaha kwa hiyo communication skills yake na wachezaji ni nzuri na rahisi.”
“Maendeleo ya Simba SC na Young Africans sio kwenye ligi ya ndani pekee kila wakati. Fikiria Young Africans baada ya miaka 25 ndiyo wameingia kwenye Robo Fainali ya CAFCL mara moja, huwezi kulinganisha na Simba SC ambaye ameingia mara tano. Kwa sababu imemaliza nafasi ya tatu kwenye ligi unaanza kuiponda Simba SC na kuidharau.
“Young Africans kama wataendelea kama walivyo na kuongeza wachezaji wazuri, wana uongozi mzuri, wana kocha mzuri na wana mashabiki wazuri, ninaimani kubwa msimu ujao wataendelea kufanya vizuri,” amesema Rage