Swaum Katambo – Katavi.
Ujenzi wa Barabara ya kiwango cha lami inayounganisha Mkoa wa Katavi na Kigoma kutoka Vikonge kwenda Luhafwe yenye urefu wa km 25 umefikia asilimia 60.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliyefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Meneja wa Wakala ya Barabara – TANROADS, Mkoa wa Katavi, Mhandisi Martin Mwakabende amesema barabara hiyo inajengwa kwa fedha za kitanzania zaidi ya bilioni 35.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika, Hamadi Mapengo na Diwani wa kata ya Tongwe Frank Kibigasi wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo kwani ilikuwa kikwazo kwa Wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo huku akimtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi kumsimamia mkandarasi ili mradi ukamilike ndani ya muda.
Aidha, Mrindoko amesema Serikali haitalala kwa kuhakikisha wananchi wanaondokana na changamoto za kulala njiani kwa kukosekana mawasiliano ya barabara.
Baadhi ya abiria waliowahi kukumbwa na kadhia ya kulala njiani kipindi cha mvua kupitia barabara hiyo wameelezea adha wanayopitia.
Mrindoko amefanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ikiwemo kukagua zoezi la ununuzi wa pamba, kuweka jiwe la msingi katika mradi wa bweni la wasichana wenye mahitaji maalum shule ya msingi Mpanda ndogo.