Boniface Gideon – Tanga.
Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tanga kimeahaidi kuwasomesha madereva wa Daladala Jijini Tanga zaidi ya 200 ambao itagharamia kiasi cha Milioni 35,000,000 kwa ajili ya kuwawezesha kupata elimu na leseni ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha ajali zinapungua.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Rajabu Abdurhaman wakati akizungumza leo wakati wa mapokezi yake yaliyofanyika kwenye ofisi za CCM Mkoa wa Tanga akitokea Jijini Dodoma ambapo Kamati kuu ya CCM Taifa ilimteua katika nafasi hiyo.
Rajabu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga alisema kwamba ameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha madereva ambao wanaendesha vyombo vya usafiri wanapata ujuzi ili kuweza kuepuka ajali wanazoweza kukumbana nazo.
“Sheria zimekuja lazima madereva wasome kwa hiyo lazima msome kweli ili muweze kuwa na halali CCM kazi yake ni kuwaunga mkono vijana ili muweze kusoma hivyo nitawaunga mkono nikitambua kwamba nyie ni wadau muhimu kwenye usafirishaji,” alisema.
Aidha aliongeza kwamba watakapokuwa wamesoma na kuendelea kufanya shughuli zao itasaidia kupungunza ajali huku akieleza ameamua kufanya hivyo kwa sababu kama kiongozi wajibu wake ni kuisaidia jamii na hayo ni maelekezo ya Rais Dkt Samia Suluhu kuwaunga mkono vijana kuweza kujikwamua kiuchumi.