Rais wa Kenya, William Ruto amevunja Baraza la Mawaziri huku akidai kuwa ataendelea kufanya mashauriano na wadau mbalimbali kuhusu masuala kadhaa yaliyoibua utata nchini humo.
Kupitia hotuba yake kwa Taifa aliyoitoa akiwa Ikulu jijini Nairobi, Ruto amesema ofisi ya Makamu wake na ile ya Mkuu wa Mawaziri hazitaathiriwa na hatua hiyo.
Amesema, “kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Ibara ya 152(1) na 152(5)(b) ya Katiba na kifungu cha 12 cha Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nimeamua kufuta mara moja mawaziri na Mwanasheria Mkuu kutoka Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Kenya isipokuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni na Diaspora.”
“Shughuli za serikali zitaendelea kama kawaida chini ya uangalizi wa makatibu wakuu wa wizara,” alisema Rais Ruto.
Hatua hiyo inakuja wakati huu ambapo utawala wake umekuwa chini ya shinikizo kumtaka kujiuzulu, kufuatia maandamano yaliyojumuisha vijana wa kizazi kipya maarufu kama Gen Z.