Swaum Katambo – Katavi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo julai 12, 2024 anatarajia kwenda mkoani Katavi kwa ajili ya kufunga kilele cha wiki ya Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho pamoja na kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa huo.
Akiwa mkoani humo leo atawasili katika uwanja wa ndege Mpanda na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja huo na atakuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha wiki ya Jumuiya ya Wazazi kitaifa ambayo rasmi itafungwa Julai 13, 2024 katika uwanja wa CCM Azimio manispaa ya Mpanda.
Aidha Shughuli zitakazofanyika katika viwanja vya Azimio ni pamoja na kufanya ufungaji rasmi wa wiki ya wazazi pamoja na kufanya mkutano wa hadhara wa kiserikali kwa maana ya kuzungumza na wananchi wote wa Mkoa wa Katavi.
Mara baada ya kumaliza shughuli za uwanja wa Azimio Rais Samia atakagua eneo la ujenzi wa kituo cha kupozea umeme kilichopo Wilaya ya Mlele ambapo umeme wa gridi ya Taifa unaotokea Tabora kuelekea mkoani Katavi.
Aidha,ifikapo Julai 14, 2024 Rais Samia atafungua jengo jipya la ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi na kufanya uzinduzi wa maghala ya kutunzia mazao mbalimbali katika eneo la Mpanda Hotel yanayo milikiwa na Taasisi ya Serikali ya NFRA baada ya hapo atazindua bandari ya Karema.
Kadhalika, Julai 15, 2024 Rais Samia anatarajiwa kukagua maendeleo ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi na kufanya mkutano wa ndani wa majumuisho na viongozi mbalimbali ndani ya mkoa kisha ataondoka kuelekea mkoani Rukwa akiwa njiani kuelekea huko atasalimiana na wananchi wa Kata ya Kibaoni Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.
Kwa upande wao wananchi mkoani Katavi wamefurahishwa na ujio wa Rais Dkt Samia Suluh Hassan kwa kuwa hakuwahi kufikia mkoani humo tokea alipoteuliwa kuwa Rais.
“Bodaboda Mkoa wa Katavi tupo pamoja na Rais wetu tunamkaribisha sana 2025 tupo pamoja nae, tunamuomba afike na Soko kubwa atuangalie, hitaji letu tunaomba aendelee kutuimarisha katika biashara zetu”amesema Athuman Juma bodaboda Soko kuu
“Tunafurahia kwa nguvu kubwa,tunataka mama akifika ajue huku ndio Tanzania kutokana na watu tunavyompenda, na ndio maana kauli yetu ni moja ukimzingua mama nasisi tunakuzingua”amesema Hamida Mussa Mkazi wa Kata ya Kashaulili
“Ujio wa Dkt Samia kwetu sisi ni kama fursa kutokana na mambo makubwa anayotufanyia sisi wanakatavi kwa sababu anakuja kuangalia fedha anazotuma kama zimefanya kazi” amesema Laurent William Mkazi wa Mtaa wa Mlimani City.