Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakulima wakiwemo wa Mkoa wa Ruvuma kubadilika na kutowauzia Mahindi walanguzi kwani Serikali imeweka vituo kwa ajili ya kununulia mahindi katika maeneo mbalimbali nchini, hususan katika mikoa inayozalisha mazao hayo kwa wingi.
Rais Samia aliyasema hayo mara baada ya kupata maelezo kuhusu usafishaji na upimaji wa mahindi unaofanywa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika kituo cha ununuzi wa mahindi kilichoko eneo la Soko Kuu, Mbinga mjini.
Amesema, “Serikali tunajitahidi kila tunapoiona changamoto tunajitahidi kurekebisha. Lakini mengine ni lazima wakulima wenyewe muamue kubadilika. Kwa mfano serikali imeweka vituo kadhaa vya kununua mahindi kwa bei kubwa. Sasa anapokuja mlanguzi kule kwako anakupa bei ya chini na wewe ukakubali kumpa isilaumiwe serikali.”
Aidha, Rais Samia pia aliwashauri Viongozi wa Wilaya hiyo kwenda kwa wakulima kuwafahamishe hatua zilizochukuliwa na Serikali na sababu ni kwanini wasiwape mahindi walanguzi bali wayalete serikalini huku akiwahakikishia soko la uhakika la mahindi yao na kuwapunguzia adha ya kuyasafirisha umbali mrefu.
Aidha, amesema ni mojawapo ya mipango ya Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuyafikisha mahindi hayo katika soko la Kimataifa kwa ajili ya manufaa ya wakulima na taifa kwa ujumla.