Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA, imetangaza kushuka kwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa Nchini zitakazotumika kuanzia leo Jumatano Oktoba 2, 2024, ambazo zimeanza kutumika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.
Taarifa iliyotolewa hii leo Oktoba 2, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk, James Mwainyekule imeeleza kuwa bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es Salaam, Petroli ni Shilingi 3,011 kwa lita, Dizeli 2,846 na Mafuta ya Taa 2,943, Mtwara Petroli 3,016 Dizeli 2,862 Mafuta ya taa 3,016 na Tanga Petroli 3,016 Dizeli 2,859 Mafuta ya taa 2,989.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, EWURA imesema bei za bidhaa za mafuta ya Petroli zitaendelea kupangwa na soko. Na kwamba wataendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.
Dkt. Mwainyekule amesema vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana, yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika na kwamba Wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.
Bei kikomo za bidhaa za mafuta ya Petroli Nchini kwa mwezi Septemba 2024 kwa rejareja katika Mkoa wa Dar es salaam Petrol ilikuwa ni Shilingi 3,140 kwa lita, Dizeli Shilingi 3,011 na Mafuta ya Taa Shilingi 3,121 huku EWURA ikisisitiza wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye mashine za (EFPP).

Hoja ya kumng'oa Mkamu wa Rais: Ulinzi waimarishwa nje ya Bunge
Mgombea urais wa upinzani jela miaka 12