Na Heldina Mwingira.

Kila mwaka Februari 14, Watu huadhimisha siku ya wapendanao, kama moja ya hatua muhimu katika safari yao ya kimahusiano lakini Mwandishi Heldina Mwingira leo katika makala hii anaangazia tukio la pete ya uchumba iliyozoeleka kwa lugha ya kiingereza kama ‘Engagement’.

Tunatambua sote kwamba kila siku, huwa inafaa kuwa ya mapenzi lakini siku hii huwa ni maalum kwa wapendanao kwa wanandoa, au watu wanaopendana wanapochunguza safari yao ya maisha, wakitambua kwamba kumbukumbu nyingi zinazohusiana na siku hii zimekuwa sehemu ya maisha yao yasiyoweza kusahaulika.

Historia yake imeanzia karne ya 3 huko Roma, ambapo alikuwapo Padri Valentine ambaye akaja kuheshimiwa kama mtakatifu hasa tarehe hiyo, lakini inaarifiwa kuwa kiongozi (Kaisari) wa kipindi hicho alikuwa Claudius II, yeye aliweka sheria kwa maaskari wote kutooa wala kufunga ndoa, kwani akiamini askari mkakamavu ni yule asiyeoa wala kuwa na familia, hivyo alipiga marufuku ndoa kwa askari.

 

Sasa Padri Valentine alipinga sheria hiyo, hivyo akaendelea kufungisha ndoa kwa siri na ndipo Mfalme Claudius II alipopata habari hizi aliamuru Valentinus akamatwe na anyongwe na ndipo Padri Valentine aliandika barua ambayo ilikuwa na salamu za kwanza za Valentine kwa binti aliyekuja kumsalimia gerezani, mwisho wa barua alihitimisha kwa maneno haya: “Kutoka kwa Valentine wako”.

Sasa kutoka hapo, Valentinus akaendelea kukumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake kuadhimishwa karibia duniani kote, na ni siku kuu ya daraja la kwanza kwa kumkumbuka Padri Valentine aliyeuawa na utawala wa kirumi sababu ya kutetea waumini wake kufunga ndoa badala ya kuishi na vimada tu.

Ikaenea sana katika nchi za magharibi na baadaye karibia sehemu kubwa ya ulimwengu na kuisherehekea kama siku ya wapendanao kinyume cha dhamira ya Mt. Valentine, hapo Watawala wa dola ya kirumi walikuwa na fikra za kueneza dola ya kirumi duniani kote na hivyo, vijana hawakutakiwa kuoa, ili wawe huru muda wote kwenda vitani kupigania nchi.

Maudhui ya siku hiyo kwa wasio wanakanisa imechukua maana nyingine ya kwamba ni siku ya wapendanao, hata kwa wasio wanandoa bali mradi wanapendana tu, kitu ambacho ni kinyume cha malengo ya mfia dini Mt. Padre Valentin aliyetaka vijana wafunge ndoa, ambayo hutanguliwa na tukio la kuvishana pete, na wengi wakiitumia siku hii muhimu.

Na katika tukio hili, huwa kuna shamrashamra nyingi, lakini kitu pekee ninachokiangazia hapa ni tukio hilo la kuvalishwa Pete kwa mwanamke ambalo mara nyingi huibua maswali na hisia ndani ya jamii husika, pale ambapo watu hujiuliza ni nani anapaswa kupiga magoti kati ya mwanaume na mwanamke pindi pete inapotolewa.

Tumeielezera Valentine ilivyoasisiwa, huku nikifahamu siku si nyingi itawadia na mengi tutashuhudia, lakini hapa mimi nataka tuone jambo moja, maana kwa mujibu wa maandiko, hasa kwa dini ya Kikristo wao kupiga magoti ni ishara ya heshima na utii na imeandikwa “enyi wanawake watiini waume zenu nanyi wanaume wapendeni wake zenu,” Waefeso 5:22-33.

Zaburi 95:6 nayo inasema, “Njooni, tusujudu, tumwabudu, tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu.” Kuinamana na kupiga magoti kwa muda mrefu kumehusishwa na ibada na heshima.”

“Kiuhalisia mwanaume ndiye anatakiwa kupigiwa goti kwani kwa tamaduni za kiafrika magoti anapiga mwanamke, na wala tusisahau tamaduni zetu wapendwa, kwani ukishaanza mpigia magoti mwanamke, moja kwa moja umempa mamlaka juu yako,” anasema Hellen Mathias ambaye ni dada aliye ndani ya ndoa.

Lakini kwenye jamii kila mtu ana mtazamo wake katika hili, Abdul ambaye ni Afisa Tehama naye anaungana na Hellen akisema, “kupiga magoti kimsingi anatakiwa apige mwanamke kuonesha Unyenyekevu kwa mwanaume. Mwanamke ndiye kachaguliwa inambidi anyenyekee kwa shukrani na upendo anatakiwa apige magoti.”

Viongozi kadhaa wa Dini nao wana maoni yao, huyu ni Mwalimu Samson kutoka Kanisa la kiroho jijini Mwanza, anasema “hiki kitu ni cha kiroho zaidi ni kwamba Pete ya uchumba kwa utaratibu wa kanisa letu huvaliwa madhabahuni na kila kitu kinachofanyika madhabahuni kina matokeo.”

“Inampasa mwanamke kupiga magoti, na suala la mwanaume kupiga magoti ni kukubali kuwa chini ya mwanamke mbele ya madhabahu ya Mungu wakati neno la Mungu linasema mwanaume ni kichwa cha familia, Mwanaume kupiga magoti huleta matokeo mabaya kama vile mke na watoto wake kutokuheshimu siku za mbeleni.”

Mtazamo wa Mwl. Samson kuhusu tukio la kuvalisha pete kuonesha mwanaume ndiye muombaji kwa mwanamke anasema, “Mwanaume haombi kuoa kwa mwanamke, mwanaume anaomba mara moja tu kukubaliwa wakati wa kutongozana na tukio la kumvalisha pete mwanamke sio kumuomba bali kumheshimisha.”

Naye Imani Oscar, Mchungaji wa kanisa la Kibaptisti la Moto Ulao anasema, “kushuka, kunyenyekea,kudeka, kulindwa kunampasa mwanamke na tabia hizi zote zinaendana na Kupiga magoti. Mwanamke apige goti na kijana asimame kwenye tukio la kuvalishwa pete, hivyo ndivyo inavyopendeza kiuhalisia.”

Katika kuendelea kujua mtazamo wa jamii, Mtaalamu wa masuala ya jinsia, Bi.Bahati Saidy yeye alisema “suala la kupiga magoti sio la lazima, labda iwe sehemu ya tamaduni kwa wahusika. Na wahusika wenyewe wanaweza kuamua tukio lao la kuvalisha pete liwe la namna gani.”

Ijapokuwa Mwanamke ameonekana kupiga magoti ni jambo sahihi, lakini wapo watu wenye mtazamo tofauti katika jamii wakisema kuwa mwanamke ndo anaombwa, kati ya muombaji au muombwaji nani anatakiwa kunyenyekea? Mwanaume anapaswa apige magoti katika tukio hilo.

Hata hivyo, kila jamii ina tamaduni zake, kuna jamii kupiga magoti kwa mwanamke inadhihirisha heshima pia zipo jamii kupiga magoti sio sehemu ya vitu vinavyotafsiriwa ni heshima, inaarifiwa kuwa tamaduni za makabila mengi ya Kitanzania mwanaume kupiga magoti ni dharau na kujishusha thamani.

Hivyo, ni muhimu kwa wanaovishana pete kupatana na kuamua tukio lao liweje. Japo mila na desturi huwa zinaingilia kati pia kwenye hili jambo na kuleta ugumu sana kupata jawabu moja linalotosheleza katika hili kwamba ni nani hasa anatakiwa kupiga magoti wakati wa tukio la kuvishana pete.

Simba yajiandaa kuelekea Qatar
Hii sio sawa kwa Steven Gerrard baada ya kutupwa daraja ya nne